Habari za Kitaifa

Natembeya akaziwa, aachiliwa kwa masharti ya kutisha

Na SAM KIPLAGAT, RICHARD MUNGUTI May 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

GAVANA wa Trans-Nzoia, George Natembeya, Jumanne aliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa taslimu baada ya kukanusha mashtaka yanayohusiana na ufisadi lakini chini ya masharti makali.

Hakimu wa mahakama ya kupambana na ufisadi ya Milimani, Charles Ondieki, alimwamuru Bw Natembeya kuweka kiasi hicho mahakamani na kuwasilisha majina ya watu wawili kumsimamia kama sehemu ya masharti ya kuachiliwa kwake.

Mahakama pia ilimpiga marufuku Bw Natembeya kuingia ofisini mwake mjini Kitale kwa kipindi cha siku 60, baada ya upande wa mashtaka kudai kuna uwezekano wake kuingilia mashahidi.

Kiongozi huyo wa kaunti alikamatwa Jumatatu na kuzuiliwa kwa siku moja kabla ya kufikishwa kortini jana asubuhi.

Bw Ondieki pia alimwagiza kutosafiri nje ya nchi bila ruhusa ya mahakama.

Gavana George Natembeya (kushoto) katika mahakama ya Milimani Jumanne akiwa na kinara wa chama cha Safina Jimi Wanjigi Jumanne Mei 20 2025. Picha|Richard Munguti

Bw Natembeya alikanusha mashtaka matatu ya ufisadi ikiwemo mgongano wa kimaslahi na kupokea fedha za umma kinyume cha sheria.

Inadaiwa Gavana huyo alipokea hongo kutoka kwa kampuni iliyokuwa ikifanya biashara na serikali ya kaunti ya Trans-Nzoia.

Kulingana na upande wa mashtaka, fedha hizo zilipitishwa kwa Bw Emmanuel Wafula Masungo, Afisa Mkuu wa Fedha wa kaunti hiyo na rafiki wa karibu wa Gavana.

Bw Masungo, ambaye ni mshitakiwa wa pili, hakuwa mahakamani wakati mashtaka yaliposomwa na mahakama ilimtaka afike kortini Mei 22.

Kesi dhidi ya wawili hao itatajwa tena Juni 3, kwa mwelekeo zaidi.

Shtaka la kwanza lililomkabili Bw Natembeya lilikuwa la mgongano wa kimaslahi kinyume na Sheria ya Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kiuchumi.

Mashtaka yalisema alipokea Sh1.1 milioni kutoka kwa Mercy Chelangat, mkurugenzi wa Lyma Agro Science Ltd na mmiliki wa Maira Stores, kampuni iliyokuwa ikifanya biashara na serikali ya Kaunti ya Trans-Nzoia.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa alipokea fedha hizo kati ya Januari 1, 2023 na Aprili 30, 2025.

Shtaka la pili lilisema alipokea Sh2.1 milioni katika kipindi hicho hicho kutoka kwa Bw Masungo, ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Easterly Winds Ltd, iliyofanya biashara na serikali ya kaunti.

Kulingana na stakabadhi za mashtaka, Bw Natembeya lijipatia manufaa ya kifedha kutoka kwa Bw Masungo.

Shtaka la tatu lilidai kuwa Bw Natembeya alipokea Sh3.2 milioni kama sehemu ya malipo yaliyofanywa kwa kampuni za Lyma Agro Science Ltd, Maira Stores na Easterly Ltd, kinyume na maslahi ya umma aliyopaswa kulinda.

Kulingana na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Bw Masungo alipokea fedha kutoka kwa wafanyabiashara na baadaye kuzipitisha kwa Gavana kupitia M-Pesa.

Baada ya kukanusha mashtaka hayo, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Renson Ingonga, alipinga kuachiliwa kwa dhamana kwa Bw Natembeya, akidai kwamba, kuna uwezekano wa kuingilia mashahidi na uchunguzi unaoendelea.

Kupitia kwa Bw Victor Juma Owiti, upande wa mashtaka ulisema kwamba, ingawa dhamana ni haki ya kikatiba, mahakama inapaswa kumnyima mshtakiwa haki hiyo pale sababu za msingi zinapowasilishwa.

“Tunapinga kuachiliwa kwa mshtakiwa kwa dhamana kwa sababu kuna uwezekano mkubwa ataingilia mashahidi, kwa sababu za usalama wa umma na uzito wa makosa haya,” alisema Bw Owiti.

 

Hakimu Charles Ondieki aliyesikiza kesi ya ufisadi dhidi ya Gavana George Natembeya. Picha|Richard Munguti

Bw Alex Akula, mwendesha mashtaka mwingine, alisema EACC inaendelea kuchunguza makosa mengine ya ufisadi dhidi ya Bw Natembeya na kutokana na yaliyotokea Jumatatu, hakufaa kupewa dhamana.

Bw Akula alitaja uharibifu wa magari manne ya EACC na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) nyumbani kwa Bw Natembeya eneo la Milimani, Kitale.

“Mashahidi katika kesi hii ni wafanyakazi wake wanaofanya kazi chini yake katika serikali ya kaunti. Anaweza kuwatisha au kuharibu ushahidi,” alisema.

Bw Akula alisema kuwa ripoti ya kabla ya dhamana inapaswa kuwasilishwa mahakamani kusaidia katika uamuzi wa dhamana.

Mpelelezi wa EACC, Bw Robert Rono, alisema katika hati ya kiapo kuwa, walikuwa wakimchunguza Bw Natembeya na watu wengine wanne kuhusu ukiukaji wa taratibu za ununuzi na malipo hewa ya Sh1.4 bilioni yaliyofanywa na Kaunti ya Trans-Nzoia kati ya mwaka wa kifedha wa 2022/2023 na 2024/2025.

Bw Natembeya, aliyekuwa akitetewa na kikosi cha mawakili 13, alisisitiza kuwa dhamana ni haki ya kikatiba na bado hana hatia hadi itakapothibitishwa vinginevyo.

Wakili wake mkuu, Bw Macharia Njeru, alisema kwa kuangalia mashtaka na hali ya kesi hiyo, ni upuuzi kumyima dhamana.

Bw Njeru alieleza kuwa taasisi huru zinatumiwa kama silaha katika mchakato wa haki, na kwamba, mchakato wa kisheria unatumika kufanikisha malengo fiche dhidi ya wale wanaochukuliwa kuwa wapinzani wa serikali.

“Hatufai kuruhusu hali ambapo mfumo wa haki ya jinai unatumika kuwaandama wapinzani,” alisema Bw Njeru.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Bw Ndegwa Njiru, ambaye alisema sababu za kupinga dhamana zilikitwa kwa tetesi na dhana tu.

Bw Ken Echesa alilalamikia jinsi gavana huyo alivyokamatwa, akisema polisi walikiuka haki zake na kutumia vibaya agizo la mahakama la kufanya upekuzi, kwa kuvunja milango ya makazi yake.