Mnyonge kunyongwa fainali ya Europa League usiku
MADRID, UHISPANIA
MACHO yote leo usiku yataelekezwa ugani San Mames jijini Bilbao, Uhispania ambapo klabu mbili nyonge za Ligi Kuu ya Uingereza -Manchester United na Tottenham Hotspur, zitakutana katika fainali ya kuwania taji la UEFA Europa League.
Mbali na kuwania taji hilo la msimu wa 2024-25, vilevile kila mmoja atakuwa akipigania tikiti ya kushiriki mechi za Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.
Timu hizi mbili zimekuwa na msimu mgumu sana kwenye ligi kuu nchini Uingereza (EPL) ambapo tayari zitakuwa kati ya klabu zitakazomaliza katika nafasi mbaya zaidi; kuanzia nafasi ya 14 na kushuka.
Kwa sasa Manchester United wanashikilia nafasi ya 16 kwenye jedwali la EPL, kwa alama 39 kutokana na mechi 37, pointi moja mbele ya Spurs.
Kwa jumla, Manchester United wamepoteza mechi muhimu kwa wapinzani 12 tofauti msimu huu wa 2024-25, na huenda mkosi huo ukawafuata dhidi ya Spurs.
Kwa upande mwingine, Tottenham wameshinda Man United katika mechi zote tatu msimu huu, mbili za EPL (3-0 ugenini na 1-0 nyumbani), kichapo kingine kikiwa cha 4-3 nyumbani katika pambano la League Cup.
Timu pekee ambayo Spurs imeshinda mara nne katika msimu mmoja ni Manchester City zilipokabiliana msimu wa 1992-93, huku timu pekee iliyowahi kushinda Man United mara nne katika msimu mmoja ikiwa Everton -msimu wa 1985-86.
Dhidi ya United msimu huu, Spurs walipata bao la kwanza kwa muda usiozidi dakika 15 kwenye mechi zote tatu, mbali na kuwalemea kwa kiasi kikubwa.
Kwa jumla ya dakika 295 na sekunde 41 katika mechi hizo tatu (pamoja na muda wa ziada, Spurs wameongoza kwa dakika 226 na sekunde 42- hiyo ikiwa asilimia 90.2 ya mchezo.
Man United wametoka nyuma na kushinda mechi sita pekee msimu huu katika mechi 58, nne wakiwa nyumbani mbele ya mashabiki wao ugani Old Trafford, ushindi mara mbili ukitokea dhidi ya timu limbukeni Southampton na Ipswich Town ambazo tayari zimeshuka daraja la EPL hadi Championship.
Kutokana na rekodi hiyo, hata kama Spurs watachukua uongozi wa mapema, licha ya kiwango kibovu cha Manchester United haimaanishi wamemaliza kazi.
Kwa upande mwingine, ushindi jijini Bilbao leo usiku utakuwa umemaliza nuksi ya Manchester United dhidi ya Spurs.
Matokeo ya timu zote kwenye EPL yamekuwa ya kuyeyuka, hasa kwa Manchester United ambayo mara ya mwisho kujipata katika hali kama hiyo ilikuwa msimu wa 1973-74, na iwapo watashindwa kuchapa Aston Villa katika mechi yao ya mwisho ya EPL, utakuwa msimu mbaya zaidi tangu wajipate katika hali kama hiyo msimu wa 1930-31 walipojiukusanyia pointi 29 pekee.
Spurs wanahitajika kushinda Brighton ili kuwa na matumaini ya kumaliza angaa katika nafasi bora, vinginevyo, utakuwa msimu mbaya sana katika historia yao ligini tangu msimu wa 1914-15 walipomaliza na pointi 36.
Mara ya mwisho fainali hii kukutanisha timu za EPL ilikuwa 2019 ambapo Chelsea ilitandika Arsenal 4-1 jijini Baku nchini Azerbaijan.