Habari za Kitaifa

Wakenya watoweka na Sh6b za hazina ya Hasla

Na EDWIN MUTAI May 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI inataka wabunge waidhinishe Sh5 bilioni zaidi kufadhili Hazina ya Hasla, huku ikibainika kuwa Sh6 bilioni hazijarejeshwa na wakopaji ambao sasa wametoweka.

Idara ya Serikali ya Biashara Ndogo na za Kati (MSMEs) iliambia Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Biashara, Viwanda na Ushirika kuwa huenda ikaomba kufutwa kwa deni la Sh6 bilioni iwapo juhudi za sasa za kuzirejesha hazitazaa matunda.

Bi Susan Mang’eni, Katibu wa Idara ya MSME, aliwaambia wabunge kuwa kati ya Sh5 bilioni 5 na Sh6.3 bilioni ziko hatarini kupotea kufuatia Wakenya milioni 10 waliokopa kukosa kulipa.

“Takriban Wakenya 10 milioni walikopa Sh500 mnamo Novemba hadi mwisho wa Desemba 2022 na hawajalipa mkopo,” Bi Mang’eni alisema.

“Tunawafuatilia na kama hatuwezi kurejesha pesa hizo, tutawazia kufuta deni la karibu Sh6 bilioni kwa watu waliokopa na kutoweka. Lakini bado hatujafikia hatua ya kufuta deni kwa sababu bado tunawafuatilia waliokosa kulipa.”

Alisema kuwa Wakenya 9 milioni kati ya wateja 25.8 milioni wa Hazina ya Hasla ni wakopaji wazuri ambao wamekuwa wakipata mikopo ya simu tangu kuzinduliwa kwa mpango huu mwaka wa 2022.

Hazina ya Halsa, mojawapo ya miradi pendwa ya Rais William Ruto, imelenga kutoa huduma za kifedha kwa Wakenya walioko chini kabisa ya ngazi ya kiuchumi, wakiwemo vijana na wanawake, kwa kutoa mikopo kwa watu ambao hawafikiwi na huduma rasmi.

Ilipozinduliwa, Hazina ya Hasla iliruhusu watu binafsi kukopa kati ya Sh 500 hadi Sh 50,000 kwa muda wa siku 14 kwa riba ya asilimia nane kwa mwaka.

Viwango vya riba vimepitiwa upya na kupandishwa kwa wakopaji wazuri na wale wanaokopa mara kwa mara.

Akizungumza mbele ya kamati inayoongozwa na Mbunge wa Ikolomani Bernard Shinali ili kutetea bajeti ya Idara ya MSME kwa mwaka wa fedha 2025/26, Bi Mang’eni aliwaambia wabunge kuwa bajeti ya Hazina ya Ujumuishaji wa Kifedha, unaojulikana zaidi kama Hazina ya Hasla, imepunguzwa hadi Sh1 bilioni kutoka Sh2 bilioni zilizokuwa zimetengwa kwenye Taarifa ya Sera ya Bajeti (BPS).

“Hazina ya Ujumuishaji wa Kifedha (Hazina ya Hasla) inahitaji Sh 5 bilioni lakini imetengewa tu Sh1 bilioni,’ Bi Mang’eni alisema wakati wa kikao Jumanne, Mei 21, 2025.

“Kwa heshima Mheshimiwa Mwenyekiti, uzoefu wa Hazina hadi sasa umeonyesha kuwa kuna hifadhidata ya Wakenya 25 milioni wanaonufaika, wenye mahitaji tofauti na yanayoongezeka ya huduma za kifedha, hali inayohitaji sisi kuendelea kuvumbua, kuendeleza na kutoa huduma za kifedha nafuu kwa watu walio chini kabisa ya mfumo wa kiuchumi, wakiwemo wale wanaohitaji mikopo, akiba, bima na uwekezaji.”

Hata hivyo, kwamba Sh6 bilioni hazijarejeshwa na wakopaji waliotoweka, ziliishtua kamati ambayo ilitaka kujua sababu ya Idara hiyo ya Serikali kuomba Sh5 bilioni zaidi kutoka kwa pesa za walipa ushuru.

“Kwa nini tukupatie Sh5 bilioni zaidi kutoka kwa walipa ushuru wakati watu wamekimbia na mabilioni ya shilingi kutoka kwa Hazina ya Hasla?” aliuliza Maryanne Keitany, makamu mwenyekiti wa kamati hiyo.

“Ikiwa Sh6 bilioni haziwezi kupatikana, kwa nini tukupatie Sh5 bilioni nyingine? Watu wa eneobunge langu walisema kuwa Sh 500 au zaidi walizokopa zilikuwa zawadi ya shukrani kutoka kwa serikali waliyoiunga mkono na kwamba hawatarudisha pesa hizo.”

Bw Shinali alimtaka Katibu kutoa sababu za msingi za kwa nini Hazina ya Hasla, ambayo ni ya mzunguko ya kima cha Sh65.5 bilioni imeshindwa kurejesha Sh6 bilioni kabla ya kuomba fedha zaidi.

Mbunge wa Kajiado Kusini Samuel Parashina na Mwakilishi wa Wanawake wa Machakos Joyce Kamene walikosoa vikali ombi la Wizara hiyo kuongezewa fedha.

“Ikiwa watu wamekopa na kutoweka, nani atarejesha pesa za umma zilizopotea? Sisi kama wabunge hatujawahi kuridhishwa na Hazina ya Hasla,” Bw Parashina alisema.