Habari

Vita ndani ya Ikulu vyaanikwa

Na KAMORE MAINA May 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

STAKABADHI mpya za mahakama zimefichua mzozo mkubwa miongoni mwa wasaidizi wa Rais katika Ikulu ya Nairobi, mkanganyiko wa mikakati ya mawasiliano, na jinsi kufadhaika kwa Rais William Ruto kwa serikali yake kupoteza mvuto kwa umma kulimpelekea kuanza harakati za kupata programu tata ya ujasusi wa kidijitali.

Bi Mary Wachuka, raia wa Canada ambaye ameshtaki wanaume wanne walio karibu na Rais Ruto akitaka fidia kwa kushindwa kutekeleza mkataba wa mfumo wa propaganda ya kidijitali, ameambatanisha mawasiliano binafsi na mmoja wa wasaidizi wa Rais yanayoonyesha mgogoro wa madaraka ndani ya Ikulu.

Bi Wachuka anasema kati ya Novemba 10, 2023 na Julai 21, 2024, alifanya mazungumzo ya kina – ana kwa ana na kwa njia ya mtandao – na maafisa wa Ikulu, akiwemo Bw Eric Ngeno, mwandishi wa hotuba wa Rais, kuhusu mfumo wa kidijitali uliopendekezwa.

Katika stakabadhi za mahakama, anadai Bw Ngeno alimweleza kuwa Rais “alielezea kwa uwazi haja ya kupata suluhisho la mawasiliano ya kidijitali lililoundwa mahsusi, kutokana na wasiwasi wa kuongezeka kwa mkanganyiko na athari hasi za mawasiliano kuhusiana na ajenda ya serikali.”

Jumanne, Bi Wachuka aliwasilisha jibu akipinga ombi la Bw Felix Koskei (Mkuu wa Utumishi wa Umma) na Katibu wa Hazina ya Taifa Bw Chris Kiptoo, waliotaka kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo.

Washtakiwa wengine ni Bw Ngeno na mfanyabiashara Bw Jayesh Saini. Mwanasheria Mkuu pia ameshtakiwa kwa niaba ya serikali.

Bi Wachuka na kampuni yake, JIPE Inc, wameshtaki Bw Koskei, Bw Kiptoo, Bw Jayesh na Bw Ngeno kwa kuvunja mkataba.

Anadai fidia ya Sh119 milioni kwa kuvunjwa kwa mkataba na Sh170 milioni kwa hasara aliyopata baada ya mpango huo kusambaratika.

Ananukuu mawasiliano ya WhatsApp ya Desemba 18, 2023 ambapo anasema Bw Ngeno alieleza kuwa mazingira ya mawasiliano yalikuwa yamevurugika, huku Bw Denis Itumbi “akiteka nyanja ya kutoa mawasiliano ya serikali na kujifanya kitovu cha mawasiliano.”

Bi Wachuka anadai kuwa Bw Ngeno alisema Bw Jayesh hakuwa sehemu ya timu rasmi ya kampeni, bali alitumia ushawishi wa kifedha na uhusiano wake “kujipenyeza”, hali iliyosababisha mkanganyiko wa ndani na hatari ya kudhuru sifa ya serikali.”

Kwa mujibu wake, Bw Ngeno aliona kuwa ushawishi wa Itumbi ulilazimisha serikali kuwa na mtazamo wa kujibu badala ya kuchukua hatua, huku muungano wa upinzani wa Azimio ukionekana kuwa na mpangilio bora.

Anamnukuu Bw Ngeno akisema: “Itumbi hangedhibitiwa, ni aibu. Jayesh aliingilia kwa sababu Azimio walikuwa wanatufunika.”

Bi Wachuka anasema Bw Ngeno alimhakikishia kuwa ufadhili wa mradi huo ungepitia “bajeti ya siri” inayosimamiwa na Hazina ya Taifa.

Alidai kuwa mnamo Novemba 22, 2023, Bw Ngeno alipanga mkutano kati yake na Bw Jayesh, ambaye alimtaja kama “mfadhili na mwenye ushawishi katika serikali hii.”

Katika mkutano huo, Jayesh alidai kuwa wabunifu wawili wa Kihindi aliokuwa ameajiri hapo awali “walitekwa nyara na kuuwa” chini ya serikali ya awali – akihusisha Mohamed Zaid Sami na Zulfikaq Ahmed Khan walioingia nchini kusaidia kampeni za Rais Ruto mwaka 2022.

Maafisa wa kikosi maalum cha polisi walihusishwa na mauaji yao tayari wamefikishwa kortini.

Katika kikao hicho, Bi Wachuka anasema Jayesh alikiri kuwa Rais alikataa mpango wa kununua mojawapo ya gazeti kubwa kwa ajili ya propaganda, na badala yake akaidhinisha programu ya kidijitali kama mbinu bora zaidi.

Baada ya kikao hicho, Bi Wachuka anasema alimweleza Bw Ngeno kuwa hataki Jayesh aongoze mradi huo na akatishia kujiondoa.

Bw Ngeno alimhimiza avumilie na akaahidi kuzungumza na Rais pamoja na Jayesh kujaribu kutatua mzozo huo.

Desemba 5, 2023, Bw Ngeno alimfahamisha kuwa alizungumza na Jayesh wakati wa ziara rasmi nchini India, ambapo Jayesh aliahidi kuwasilisha bajeti ya programu kwa Rais na kuwa angeiunga mkono.

Lakini Desemba 12, 2023, mvutano ulizidi na Ngeno na Jayesh walikorofishana, kila mmoja akimlaumu mwenzake kwa kuchelewesha mradi.

Ngeno alimtumia Wachuka jumbe za hasira, akimkosoa Jayesh kwa “kiburi, ukaribu wake na Rais, na kuwa mpango wa kujinufaisha kwa mradi huo.”

Bi Wachuka anamnukuu akisema: “Alijifanya mtaalamu na mwenye mamlaka… Nashindwa kuvumilia, nitamwambia moja kwa moja.”

Baada ya mgogoro huo, Bw Ngeno aliamua kumwendea Rais moja kwa moja, na baadaye alimfahamisha Bi Wachuka kuwa Rais aliidhinisha mradi huo na akaagiza utekelezwe mara moja.

Ngeno alimwambia kuwa Rais alitaka kuupitia mradi huo asubuhi kabla ya kuelekea Eldoret kwa likizo ya Krismasi.

Kukabiliana na hoja ya kuwa hakukuwa na mkataba wa kisheria, Bi Wachuka anasema alikutana na Mkurugenzi Mkuu wa Uwekezaji wa Umma Bw Kibet mnamo Machi 11, 2024, katika Hazina ya Taifa, ambapo aliambiwa kuwa serikali ilikuwa tayari kufadhili mradi huo.

Mara baada ya kuthibitishwa kwa maneno, Wachuka, Ngeno na wanakandarasi wake walifanya mkutano wa mtandaoni kupanga vipengele vya kiufundi vya mfumo huo.

Katika mkutano huo, Ngeno alifichua kuwa Rais alitoa maagizo ya kuongeza vipengele vya “mashambulizi ya kidijitali” dhidi ya wanasiasa na mashirika ya kijamii.

Mnamo Desemba 29, 2023, Wachuka anasema Ngeno alimwandikia ujumbe mwingine wa WhatsApp akimfahamisha kuwa “wakubwa wameidhinisha” na fedha zimepatikana.

Kwa mujibu wa Bi Wachuka, maafisa muhimu waliotajwa kuwa na jukumu kubwa ni Katibu  wa Hazina ya Taifa, Mkuu wa Utumishi wa Umma, na Mkurugenzi Mkuu wa Uwekezaji wa Umma.