Habari

Wacheni kukamata viongozi kama magaidi, Salasya aambia serikali

Na STEPHEN MUNYIRI May 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, amekosoa vikali mbinu zinazotumiwa na polisi kuwakamata Wakenya, akisema kuwa mbinu hizo zinazofanana na operesheni za makomando na za kigaidi ni “matumizi ya nguvu kupita kiasi” isiyo ya lazima.

Mbunge huyo alisema viongozi ni raia wanaoheshimu sheria na hata wanaweza kutii “wito kupitia mitandao ya kijamii” ya polisi

Akizungumza Jumatano na wakazi wa mji wa Karatina katika Kaunti ya Nyeri alipofanya ziara ya ghafla, Salasya ambaye anajiita mwenyekiti wa vijana aliwahimiza vijana hasa kizazi cha Gen Z kujipanga kuchukua uongozi wa nchi baada ya uchaguzi wa 2027.

Alisema vijana ndio watakaowaletea Wakenya uongozi wa maendeleo, akitoa mfano Rais wa Burkina Faso Ibrahim Traoré, kama kiongozi kijana mwenye uwezo wa kubadilisha Afrika.

“Sisi ndio tutakaoamua nani ataiongoza Kenya. Wakati umefika sasa wa sisi kuchukua uongozi wa nchi hii na kuibadilisha,” alisema.

Mbunge huyo alisimulia jinsi alivyokamatwa mjini Nanyuki akisema ni mbinu “hatari na ya kiholela.”

“Maafisa waliokuja kunikamata hata hawakujua walikuwa wameagizwa kufanya hivyo kwa sababu gani. Walifyatulia risasi gari letu. Hii ingeweza kusababisha janga. Ni kwa neema ya Mungu tu hakuna aliyejeruhiwa,” alisema.

Bw Salasya alikamatwa kuhusiana na madai ya uchochezi kutokana na chapisho linalodaiwa kuwekwa kwenye mojawapo ya akaunti zake za mitandao ya kijamii.

“Nilikamatwa kama gaidi kwa sababu tu ya kitu kilichoandikwa kwenye mitandao ya kijamii,” alisema.

Alitoa wito kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhakikisha inawapa maelezo ya kina maafisa wake kabla ya kuwatuma kutekeleza majukumu, akionya kuwa mawasiliano duni  yanaweza kukiuka haki za binadamu na kuchochea taharuki.

“Uongozi wa DCI lazima uhakikishe kuwa maafisa wao wa chini wanaelewa kazi wanayoifanya. Hatuwezi kuendelea kuishi katika nchi ambako watu wananyanyaswa na kutishwa na taasisi za serikali,” alisema.