Mwanafunzi ashtaki shule kwa kujeruhiwa sikio
MWANAFUNZI ameshtaki Shule ya St Bakhita, Nairobi, akidai kuwa taasisi hiyo ilishindwa kumlinda baada ya kudaiwa kuadhibiwa na mwalimu mnamo Machi, jambo lililosababisha jeraha kwenye sikio lake.
Kupitia kwa baba yake, mwanafunzi huyo ambaye jina lake limefichwa kwa ulinzi wake, alisema alifinywa na mwalimu wake wa Kiswahili Machi 19, tukio ambalo limemwacha na mshtuko na woga.
Baba huyo ameshtaki shule hiyo, bodi ya wakurugenzi, mwalimu mkuu James Ogweno pamoja na Bw Fredrick Manyasa, mwalimu anayedaiwa kumjeruhi mwanafunzi huyo.
Bw G.O. alisema katika stakabadhi za mahakama kuwa “shambulio hilo lilikuwa la makusudi na lililenga kumdhuru mtoto huyo.”
“Mlalamishi anadai kuwa mtoto huyo anaonekana wazi kuwa amepatwa na mshtuko, anaogopa, amejitenga na hulia bila kukoma kila mara anaposikia jambo lolote linalohusiana na shule,” alisema Bw G.O.
Kesi hiyo itatajwa Juni 17 mahakama itoe mwelekeo.
G.O. alisema shule hiyo ilishindwa kutekeleza wajibu wake wa kumlinda mtoto huyo dhidi ya mateso au adhabu ya kinyama na udhalilishaji, pamoja na kuhakikisha mazingira mazuri kwa mtoto huyo kama mwanafunzi.
Alisema tukio hilo limemfanya mtoto huyo kuomba ahamishwe na kutafuta usaidizi wa ushauri nasaha.
“Mtoto anahudhuria vikao vya ushauri nasaha ili kusaidia hali yake ya kihisia,” alisema baba huyo.
Mlalamishi anadai kuwa haki na uhuru wa mtoto huyo zilikiukwa, ikiwemo uhuru dhidi ya mateso, adhabu ya kikatili, na udhalilishaji.
Anadai fidia ya jumla na maalum, ikiwa ni pamoja na Sh18,618 zilizotumika kwa matibabu na gharama nyinginezo.
“Tunaomba mahakama itoe tamko kuwa vitendo dhidi ya mtoto huyo vilikuwa kinyume cha Katiba, haramu, vya kudhalilisha na vya kikatili, na hivyo basi washitakiwa wawajibike,” alisema G.O.
Anataka pia agizo kutoka kwa mahakama kuamuru shule hiyo kulipia gharama za matibabu ya sasa na ya baadaye hadi mtoto huyo apone kabisa katika hospitali atakayochagua.
Mzazi huyo alieleza kuwa shule hiyo ilijitolea kumpatia mtoto huyo huduma za ushauri nasaha na msaada wa kihisia bila malipo yoyote.