Wakenya, Watanzania wakomoana siku mbili mfululizo kuhusu kufurushwa kwa watetezi wa haki
NIPE nikupe kati ya Wakenya na Watanzania iliendelea kushamiri Jumatano nje na kwenye mitandaoni kufuatia kufurushwa kwa baadhi ya Wakenya walioenda Tanzania kufuatilia kesi dhidi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu.
Isitoshe, wanaharakati wa kutetea haki nchini Kenya walikasirishwa na hatua ya serikali ya Tanzania kuendelea kumzuilia mwanaharaka wa Kenya Boniface Mwangi na wakili raia wa Uganda Agatha Atuhaire tangu Jumapili walipodaiwa kukamatwa na polisi dakika chache baada ya kuwasili nchini humo.
Chini ya mwavuli wa Kongamano la Mapinduzi, wanaharakati hao sasa wametoa makataa ya saa 24 kwa Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan aamuru kuachiliwa kwa Bi Mwangi na Bi Agatha la sivyo wateke ubalozi wa nchi hiyo jijini Nairobi.
Aidha, wametisha kuandamana hadi Tanzania kwenyewe kushinikiza kuachiliwa huru kwa wawili hao.
“Wenzetu Agatha na Boniface wangali wanazuiliwa na serikali ya Tanzania, hatuwezi kuwasiliana nao kwani wamepokonywa simu,” akasema Don Githuku Jumanne.
“Tunampa Suluhu makataa ya saa 24 awaachilie la sivyo tutateka Ubalozi wa Tanzania. Na hiyo haitoshi, tutaenda Tanzania!” akaongeza.
Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la Vocal Africa Hussein Khalid naye alimtaja Rais Samia kama kiongozi “dhalimu” na “dikteta” asiyeheshimu haki za kimsingi za kiraia.
“Sharti Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aheshimu haki za kiraia. Huu udikteta hauna nafasi katika ulimwengu wa sasa. Sharti amwachilie huru Boni na Agatha,” akaeleza walipofika nje ubolozi wa Tanzania Nairobi. Mkewe Mwangi, Njeri Mwangi, aliyeandamana nao, alionekana akibubujikwa na machozi hadharani.
Jumatano, Wakenya na Watanzania waliendelea kurushiana cheche mitandano kuhusu suala hilo, ambalo sasa linatishia kuathiria mahusiano kati ya raia wa mataifa hayo jirani.
Wanablogu Cornelius Rono, Torome 254, @Ikinda Kani walimkashifu Rais Samia wakimtaja kama dikteta mpya eneo la Afrika Mashariki.
“Siku zake uongozini zinahesabika. Amemtupa gerezani Tundu Lissu. Akamfurusha Martha Karua aliyefika kumtetea kiongozi huyo, na hakumsaza Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga na wengine,” akasema Torome 254 kupitia mtandao wa X.
Naye @Ikinda Kani akafoka; “Ewe Mama Samia, hauna aibu ukimkosea heshima Martha Karua ilhali Watanzania wamejaa huku Kenya. Hapa Nairobi wanaendesha biashara za bidhaa haramu, zingine zikiwa zile zinazodhoofu afya ya binadamu!
Naye Rono akaonekana kusifia Wakenya akisema; “Ndani ya saa 24 Wakenya wametimiza yale Watanzania walifeli kufanya ndani ya miaka 65. Ama kwa kweli Wakenya ni viumbe spesheli kutoka kwa Mungu. Kutoka Kenya unaenda mbinguni.”
Nao baadhi ya Watanzania walimsifia Rais Samia na uongozi wake wakisema ni sahihi.
“Rais Samia anatosha sana. Amedhihiri uongozi imara, wenye hekima na maono mazuri kwa taifa letu. Ana kila haki ya kukinga Tanzania isiharibiwe na kuvurugwa na wanaharakati nje haswa Kenya,” akasema @Muhaluri1.
Isitoshe, kanda moja ilisambazwa mitandaoni ikiwaonyesha kundi la akina mama Watanzania wakisifia kiwango cha masomo cha Rais Samia kama kielelezo kwamba ni kiongozi bora.
“Rais Samia ana shahada mbalimbali vya hadi kiwango cha udaktari alivyopata kutoka vyuo vikuu vya Dar es Salama, Zanzibar. Ankara nchini Uturuki, London Uingereza kati ya zingine. Vile vile, amewekwa kwenye orodha ya Forbes kuwa miongoni mwa wanawake 100 wenye ushawishi mkubwa duniani,” mmoja wa wanawake hao akasikika akisema.
Mnamo Jumatatu, Mei 19, Rais Samia alisema serikali yake haitawaruhusu wanaharakati kutoka mataifa ya kigeni kuingia Tanzania kuleta vurugu.
“Wameharibu kwao na hatutawaruhusu kuja huku kwetu kuvuga amani,” akasema alipoongoza uzinduzi wa Sera ya Kigeni ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Alisema hayo baada ya serikali yake kuwafurusha kiongozi wa Peoples’ Liberation Party (PLP) Martha Karua, wanaharakari Lynn Ngugi na Gloria Kimani, aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga, Bw Khalif, mwanaharakai Hanifa Adan.
Wakenya hao walipania kuhudhuria kikao cha mahakama inayoshughulikia kesi dhidi ya Bw Lissu.