Wakazi wa Mukuru walia ‘wageni’ walipewa nyumba za bei nafuu
SIKU moja tu baada ya Rais William Ruto kukabidhi rasmi nyumba 1,080 zilizokamilika katika mradi wa nyumba za bei nafuu wa Mukuru kwa wamiliki wake, vigezo vilivyotumika kugawa nyumba hizo vimeanza kutiliwa shaka.
Wakazi wa Mukuru kwa Njenga, ambao walitarajiwa kuwa walengwa wa mradi huo, wameeleza kusikitishwa kwao na utekelezaji wa mpango huo.
Wakati wa kukabidhi nyumba hizo, Rais Ruto alisifu serikali yake kwa kufanikisha ujenzi wa vyumba vya bei nafuu kwa watu waliokuwa wakiishi kwenye mitaa ya mabanda.
Miongoni mwa waandamanaji walioingia barabarani Jumatano ni Jane (jina la pili limehifadhiwa kwa sababu za kiusalama).
Licha ya kupitia mchakato wote ilivyohitajika na Bodi ya Nyumba za Bei Nafuu kupitia tovuti ya Boma Yangu, hakupata nyumba aliyoomba.
“Nina kadi hapa. Unaweza kuona maelezo yangu na namba ya nyumba niliyopangiwa. Lakini bado niko hapa kwenye mabanda kwa sababu sikupata nyumba. Nataka kwenda kwa ofisi ya chifu kuuliza kwa nini sikuchaguliwa,” alisema.
Jane alisema alifahamu kuhusu hafla ya Rais kupitia vyombo vya habari, jambo lililomfanya kuhoji uwazi wa mchakato huo wa kutoa nyumba.
“Sijui nyumba hizi zinatolewaje. Tulipewa hizi kadi tukaambiwa tusubiri hadi watakapowasiliana nasi kuhusu siku ya kuhama,” aliongeza.
Kwa mujibu wake, watu waliopatiwa nyumba hizo katika mtaa mpya wa Mukuru hawatoki kwenye mabanda ya Mukuru.
“Nimesikia watu wawili tu waliopata nyumba hizo lakini wenzangu wengine wote hawakupata. Wengi waliopata ni wageni, watu kutoka South B na maeneo mengine.”
Veronica Katundu, ambaye ameishi mabandani kwa zaidi ya miaka 20, alisema serikali haikuwapa taarifa za kutosha kuhusu mradi wa nyumba za bei nafuu, hivyo walijikuta wameachwa nje kwa sababu ya ukosefu wa taarifa.
“Sikuomba hizo nyumba kwa sababu sikupata taarifa za kutosha. Labda nitaomba nyumba ya chumba kimoja nikizipata taarifa vizuri,” Bi Katundu alisema, na kuongeza kuwa alikuwa miongoni mwa watu waliokwenda kwenye hafla ya Rais na kushangaa kuona nyuso mpya ndizo zilizopewa nyumba hizo.
“Tumeona nyuso mpya pale, lakini serikali inapaswa kuwazingatia watu waliokuwa wakiishi katika mabanda haya kwa miaka mingi.”
Vijana waliozungumza na vyombo vya habari walisema kuwa “mahsla” wa kweli waliokuwa wakilipa hadi Sh2,000 kama kodi ya nyumba katika mabanda hawawezi kumudu kodi ya Sh3,900 ya chumba kipya cha nyumba za bei nafuu.
“Baadhi yetu hatuna ajira, maisha ni magumu. Watu wanaopewa hizo nyumba si wale tunaowafahamu, huo ni uhusiano mwema tu. Rais anapaswa kufahamu kuwa sisi sote tuna haki ya kuishi,” alisema Ali Mohamed.
Aliomba serikali kuwaruhusu wakazi wa mitaa ya mabanda kuishi kwa amani bila vitisho vya kufurushwa au kulazimishwa kuhamia kwenye nyumba ambazo hawawezi kumudu.
“Hauwezi kunipa nafasi halafu unaniambia hapa ndipo nyumbani, wakati siwezi hata kufuga kuku au paka ndani. Tunataka amani huku mtaani. Tunajua utamu wa maisha ya huku kwa sababu hapa ndipo nyumbani kwetu,” alisema Bw Mohamed.
Kauli yake iliungwa mkono na Nur Hassan, ambaye alisema kuwa mchakato haukuwa wazi, na kumtaka Rais kuingilia kati kuhakikisha kuwa watu wa kweli kutoka maeneo ya mabanda ndio wananufaika.
“Hao watu walipewa nyumba si wa mabandani. Tunataka mchakato uanze upya, watu wachujwe ipasavyo kabla ya kupewa nyumba ili walio halali wapate. Serikali itafute utaratibu mzuri,” alisema Bw Nur.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Nyumba za Bei Nafuu, Sheila Waweru, watu waliokuwa wamechaguliwa lakini hawakupata nyumba watazingatiwa katika awamu inayofuata.
“Wale waliokuwa wamefanikiwa lakini hawakupata nyumba wamewekwa kwenye orodha ya kusubiri. Hii inamaanisha kwamba unaweza kuomba awamu ya pili au kuchagua mradi mwingine unaoendelea kwenye mfumo wetu,” alisema Bi Waweru.