Mashirika 20 ya afya kukwama kwa kutotengewa pesa katika bajeti
TAKRIBAN mashirika 20 ya serikali katika sekta ya afya yanatarajia kupoteza karibu Sh1 bilioni katika mwaka wa fedha unaoanza Juni.
Kupunguzwa kwa fedha kutafanya kuwe vigumu kwa mashirika haya kulipa wafanyakazi wao na kugharamia mahitaji ya kila siku.
Ikiwa mashirika haya hayataweza kuendeleza shughuli zake za kawaida, huduma za afya kwa Wakenya huenda zikaathirika pakubwa.
Mashirika haya ambayo ni sehemu ya yaliyo na uhuru wa kujitegemea yanatoka katika Idara ya Serikali ya Afya ya Umma na Viwango vya Kitaaluma.
Kati ya mashirika hayo 20 ya umma, sita hayakupokea hata senti moja katika rasimu ya bajeti ya mwaka wa 2025/26 ambayo kwa sasa inakaguliwa na kamati za Bunge.
Mashirika yaliyoathiriwa ni pamoja na Bodi ya Dawa na Sumu (PPB), Baraza la Uuguzi la Kenya, Bodi ya Usimamizi wa Taarifa na Rekodi za Afya, Hazina ya Kudhibiti Tumbaku, Bodi ya Kudhibiti Tumbaku, na Bodi ya Wataalamu wa Maabara za Afya Kenya.
Ni Maabara ya Kitaifa ya Kudhibiti Ubora pekee ndiyo imepokea takriban Sh10.7 milioni ikiwa ni mara ya kwanza kufadhiliwa baada ya kutopokea chochote kwenye Taarifa ya Sera ya Bajeti mwezi Februari.
Katika mawasilisho yake kwa Kamati ya Bunge ya Afya inayoongozwa na Mbunge wa Seme James Nyikal, Waziri wa Afya Aden Duale aliomba kamati hiyo kufikiria upya bajeti yao, hasa kwa mashirika haya.
“Ukosefu wa ufadhili wa kutosha kwa mashirika haya, hasa hospitali za rufaa, Chuo cha Mafunzo ya Matibabu Kenya na Mashirika ya Udhibiti pamoja na kuanzishwa kwa hospitali mpya maalum, kunahitaji kuongezwa kwa bajeti ili kuajiri na kudumisha wahudumu wa afya, kwa lengo la kuhakikisha utoaji wa huduma bora za afya kwa Wakenya katika miundombinu ya kisasa ya afya chini ya idara hii ya serikali,” alisema.
Katibu wa Idara ya Afya ya Umma Mary Muthoni aliambia wabunge kuwa pendekezo la kupunguza bajeti kwa asilimia 20 au zaidi litaathiri shughuli za kila siku za mashirika hayo.
“Ninaomba kamati iingilie kati na kufikiria upya pendekezo hili na kutengea pesa mashirika hayo, angalau kuyawezesha kulipa mishahara ya wafanyakazi wao,” alisema.