Habari

Gachagua kutumia mamilioni kuzindua rasmi chama chake cha DCP Juni 3

Na Benson Matheka May 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA naibu rais Rigathi Gachagua atazindua rasmi chama chake cha Democracy for the Citizens (DCP) mnamo Juni 3, 2025.

Tarehe hiyo ilifichuliwa katika barua ambayo chama kimeomba kutumia Ukumbi wa Uwanja wa Michezo wa Kasarani kwa hafla hiyo, inayotarajiwa kubadilisha taswira ya kisiasa nchini.

Ombi hilo lililowasilishwa Mei 20, lilionyesha maandalizi ya kina yaliyofanywa ili kuhakikisha mafanikio ya tukio hilo.

“Ninaandika kuomba rasmi kutumia Ukumbi wa Kasarani Gymnassium kwa uzinduzi rasmi wa chama chetu, unaopangwa kufanyika Jumanne, Juni 3, 2025, kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni,”  ilisema sehemu ya barua hiyo.

“Hafla hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na watu takriban 5,000, wakiwemo wanachama wa chama, wafuasi, wageni waalikwa, na wanahabari,” iliendelea.

Kulingana na chama hicho, ukumbi huo, ambao utagharimu Sh3.7 milioni, utatumika kwa hotuba na  burudani, kwa lengo la kufichua msingi na uongozi  wa chama kwa umma..

“Tunaomba kwa heshima tupatiwe taarifa kuhusu upatikanaji wa ukumbi katika tarehe husika, utaratibu wa kuutumia, pamoja na gharama na mahitaji yanayohusiana na hatua hii,” barua hiyo iliendelea.

Usimamizi wa ukumbi ulithibitisha  kuwa utapatikana na kiasi ambacho chama kilihitajika kulipa.

Ada ya kukodi  ukumbi  itagharimu chama Sh1.4 milioni, pamoja na gharama nyingine kama vile uwekaji chapa, kutumia chumba cha wageni wa heshima (VIP), ada ya usafi, eneo la maonyesho, matangazo ya moja kwa moja, na matumizi ya taa za mwangaza, jumla ikiwa Sh3.7 milioni.

Huu utakuwa ni uzinduzi rasmi wa chama hicho, baada ya kutambulishwa kwa mara ya kwanza katika makao makuu ya chama huko Lavington, Nairobi, mnamo Mei 15.