Madhila ya Boniface Mwangi: Martha Karua aindikia AUC
KIONGOZI wa chama cha People’s Liberation Party (PLP) Martha Karua amewasilisha malalamishi kwa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) kuhusu kile alichokitaja kama “kudorora kwa utawala wa sheria” nchini Tanzania.
Kwenye barua, aliyoiwasilishwa Alhamisi Mei 22, 2024 na ambayo nakala yake alituma kwa makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Bi Karua ametaja kuteswa kwa mwanaharakati Boniface Mwangi na wakili raia wa Uganda Agather Aruhaire kama kielelezo kukithiri mwenendo wa ukiukaji haki nchini Tanzania.
“Kuzuiliwa akwa Bw Mwangi na Bi Atuhaire kulitokea baada ya kuzuiliwa na kufurushwa kwa raia sita wengine wa kigeni waliowasili katika uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere kutaka kuhudhuria kikao cha mahakama kuhusu kesi inayomkabili kiongozi wa upinzani Tundu Lissu. Miongoni mwa waliozuliwa ni mimi na Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga,” akaeleza Bi Karua ambaye ni Waziri wa zamani wa Haki na Masuala ya Kikatiba.
Mwanasiasa huyo, ambaye ni Wakili Mkuu, alisema kitendo hicho cha serikali ya Tanzania ni kinyume na viwango hitaji vya haki za kibinadamu nchini humo na kimataifa.
“Aidha, kitendo kama hicho kinashabihiana na mwenendo hatari wa utekaji nyara, mateso na mauaji ya kiholela yanayoendelea katika ukanda huu wa Afrika Mashariki,” akaongeza.
Bi Karua sasa anaitaka AUC kuingilia kati suala hilo na iilazimu Tanzania kukomesha vitendo vya ukiukaji wa haki inavyowatendea wakosoaji wake utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan na wageni wanaodhaniwa kuwasawiri kuunga mkono upinzani nchini humo.
Awali, mnamo Alhamisi, Bw Mwangi aliachiliwa na maafisa wa usalama wa Tanzania na kusafirishwa hadi eneo la Ukunda, kaunti ya Kwale ambako alipatikana.
Mwanaharakati huyo alikuwa amedhoofika kimwili huku akilalamika kuwa aliteswa na walinda usalama wa Tanzania tangu Jumapili wiki jana alipozuliwa dakika chache baada ya kuwasili nchini humo.
Baada ya kupatikana, Bw Mwangi alisafirishwa hadi Nairobi kwa matibabu.
“Ni mchovu na inaonekana mwenye maumvi. Maafisa wa tume na wadau wengine wanaendelea na mipango ya kumsafirishwa hadi Nairobi kwa matibabu,” Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNCHR) ikasema kwenye taarifa.
Bw Mwangi aliachiliwa baada ya serikali ya Kenya kuandika barua ya malalamishi kwa serikali ya Tanzania kuhusu madhila ya Mkenya huyo baada ya kukamatwa kwake.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Kenya ilielezea kusikitishwa kwake kwamba tangu kukamatwa kwa mwanaharakati huyo Jumapili, maafisa wa ubalozi wa Kenya jijini Dar es Salama hawaruhusiwa kumfikia licha ya kuomba mara kadhaa kufanya hivyo.
Wizara hiyo ilielezea hofu kuhusu hali yake ya afya na hali yake kwa ujumla kwani hamna aliyefahamu mahala ambako Bw Mwangi alikuwa akizuiliwa.
“Wizara inaelezea hofu kwamba, baada ya kuomba mara kadhaa, maafisa wa serikali ya Kenya wamezuiliwa kumfikia Bw Mwangi. Aidha, kuna wasiwasi kuhusu hali yake ya kiafya ikizingatiwa kuwa haijulikani aliko,” ikaeleza barua kutoka kwa Wizara ya Masuala ya Kigeni.
Wizara hiyo ilisema kuwa kuzuiliwa kwa Bw Mwangi ni kinyume matakwa ya Mkataba wa Vienna kuhusu Mahusiano ya Kidiplomasia ya 1963 ambao imeratibiwa na Jamhuri ya Kenya na Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Kulingana na mkataba huo, maafisa wa kibalozi huruhusiwa kumtembelea raia yeyote na taifa fulani aliye gerezani, kizuizini na anazuiliwa katika nchi ya kigeni kwa kosa lolote lile.