Ajabu wanawake wakikimbilia wanyama kipenzi badala ya kuzaa
KUNA mapinduzi ya kimya yanayoendelea miongoni mwa wanawake wa Kenya huku wakichagua wanyama kipenzi badala ya kupata watoto. Hii ni kinyume kabisa na tamaduni za jadi ambazo zilimchukulia mwanamke kuwa hajakamilika ikiwa hana mtoto.
Siku hizi, wanawake wengi wanafanya maamuzi ya makusudi ya kutokuwa mama, si kwa sababu hawawezi kupata watoto, bali kwa sababu hawataki. Badala ya watoto, wanakumbatia paka na mbwa. Badala ya chupa za watoto, nguo na vinyago, wanawekeza katika chakula cha wanyama, vifaa vya kuondoa manyoya, na mabakuli ya kulishia. Wanyama wao wanapendwa, wanatunzwa, na kwa njia nyingi, wanachukuliwa kama watoto.
Jane Njeri, mwenye umri wa miaka 43, ni mhadhiri wa chuo kikuu na mama wa paka tisa. Alipokuwa mdogo, alitarajia kuolewa akiwa na umri wa miaka 25 na kupata watoto watatu au wanne. Lakini maisha yalichukua mkondo tofauti.
“Ni uamuzi niliofanya kwa muda. Baada ya masomo yangu ya chuo kikuu, nilihusiana na watu wachache lakini sikufanikiwa. Nilirudi kusoma nikapata Shahada ya Uzamili, kisha Shahada ya Uzamivu. Mahusiano hayakuwa kipaumbele tena,” anasema.
Akiwa mhadhiri, anashuhudia changamoto nyingi wazazi wanazopitia kulea watoto. Anasema watoto wanahitaji nguvu nyingi na mara nyingine huleta hasira kuliko furaha. “Nimeamua kuwa sawa na maisha yangu bila watoto, na hali yangu ya maisha ni nzuri,” anasema.
Mama yake hapendezwi na uamuzi wake na mara nyingi humwambia, “Laiti ungelipenda mama yako kama unavyowapenda paka wako.” Jane hutumia takribani Sh10,000 kwa mwezi kwa paka wake, na hadi Sh30,000 ikijumuisha gharama za matibabu.
Eva Mutua, wakili, ana mbwa watatu: Max, Joe, na Ruby.Mbwa hawa walimsaidia kupona baada ya kufiwa na mama yake. “Walikuja maishani mwangu polepole na kunisaidia kuponya huzuni yangu,” anasema.
Eva alipanga maisha yake mapema – alitarajia kuwa ameolewa na kupata watoto kabla ya kufikisha miaka 32. Lakini baada ya kusoma India na kuishi Uingereza, mahusiano yake hayakufaulu. “Nilijikuta sina mtu sahihi wa maisha na nilifanya amani na hali hiyo,” asema.
Tofauti na Jane, mama yake Eva alimwelewa na hakumpa presha. “Watu walimwambia anilazimishe kupata mtoto, lakini alisema, ‘Nitabaki kumlea mimi huyo mtoto.’”
Eva huwachukulia mbwa wake kama watoto wake wa kweli. “Ninawavalisha na ninawapeleka kuoshwa.”
Aliomba Mungu kabla ya kuamua kutopata watoto. “Niliomba Mungu anipe mtu wa maisha ambaye naweza kupata naye watoto. Hilo halikutokea na nikaomba nguvu za kuikubali hali hiyo kwa amani.”
Stephen Karimi, mwanasaikolojia, anasema kuchagua wanyama badala ya watoto kunasababishwa na sababu za kihisia, kiuchumi na hata kibaolojia.
“Hauwezi kuchukua nafasi ya kipekee ambayo mtoto huleta, lakini unaweza kupata uhusiano wa karibu kupitia wanyama vipenzi” asema.
Anabainisha kuwa tafiti zinaonyesha kuwa wanyama hupunguza upweke, na hisia hasi maishani. “Wanyama ni chanzo cha msaada wa kihisia na walinzi wa upendo.”
Hata hivyo, anaonya kwamba wanyama hawawezi kuchukua kabisa nafasi ya mtoto wa binadamu.