Habari

Babu Owino sasa ni wakili, aahidi kutetea wanyonge

Na Cynthia Makena May 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, alikuwa miongoni mwa mawakili 609 waliodhinishwa kuhudumu katika Mahakama Kuu katika sherehe iliyoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome.

Jaji Mkuu Koome aliwaambia mawakili wapya waingie kwenye taaluma hiyo kwa kuongozwa na misingi ya ujasiri, uadilifu, na huduma kwa wananchi.

“Joho nyeusi mnayovaa si ishara ya hadhi bali ni ishara ya uaminifu. Kama mawakili wapya, fikirieni jinsi mtakavyotumia sauti na ujuzi wenu kuleta haki karibu na wananchi. Msimamie haki kwa ujasiri. Kutakuwa na shinikizo la kukubali hali isiwe sawa, kuangalia upande mwingine au kukaa kimya lakini nawahimiza msikate tamaa. Zungumzeni kwa niaba ya wasio na sauti, simameni imara kwa yale yaliyo sawa. Hili ndilo Kenya inahitaji,” alisema Jaji Mkuu Koome.

Alisisitiza nafasi muhimu wanazopewa mawakili katika kuimarisha demokrasia, kulinda haki na kuhakikisha haki inapatikana kwa kila Mkenya.

Jaji Mkuu pia alikiri mabadiliko katika sekta ya sheria, ikiwemo ongezeko la matumizi ya majukwaa ya kidijitali na umuhimu wa ubunifu katika sheria.

“Mawakili wana jukumu la msingi katika kuimarisha demokrasia, kulinda haki na kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa Wakenya wote. Kadiri sheria inavyoendelea kubadilika, tunapaswa kukumbatia ubunifu na kutambua ushawishi unaoongezeka wa majukwaa ya kidijitali katika kazi uanasheria,” alisema Jaji Mkuu Koome.

Bw Owino alitaja ukosefu wa usawa na unyanyasaji alioshuhudia akiwa mdogo  mtaani Nyalenda, Kisumu, kama kichocheo chake kikuu cha kusoma sheria na hatimaye kuhitimu kuwa wakili wa Mahakama Kuu.

 “Nikiwa mtaani Nyalenda, niliona kwa wasiwasi mkubwa unyanyasaji na kunyanyaswa kwa Wakenya wa kawaida mikononi mwa maafisa wa serikali, mara nyingi bila kujua haki zao za kikatiba,” Bw Owino aliwaambia waandishi wa habari.

Tovuti rasmi ya Bunge, inaonyesha kuwa Mbunge huyo ana Shahada ya Sayansi (Actuarial Science), Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Actuarial na Shahada ya Sheria.

Bw Owino alionya serikali na kuahidi kuwakilisha Wakenya hasa kupinga sera zinazoweza kuhatarisha maisha yao.

“Serikali inapaswa kujiandaa kwa hoja kali zaidi katika kutetea Wakenya – bungeni na sasa mahakamani. Tarajieni hatua za kisheria zinazolenga kupunguza gharama ya maisha, kuunda ajira na kuwajibisha mifumo,” alisema.