Kindiki- Tutaendelea kumwaga pesa kwenye harambee kote nchini
NAIBU Rais Kithure Kindiki ametetea mpango wa uwezeshaji wa kiuchumi ambapo wanasiasa wanatoa mamilioni ya pesa kwa wafanyabiashara kote nchini, akisema ni njia bora ya kuimarisha biashara zisizo rasmi.
Katika miezi miwili iliyopita, Profesa Kindiki na viongozi wengine wa Kenya Kwanza wamezunguka nchi nzima na kufikia sasa wametoa zaidi ya Sh100 milioni kwa vikundi vya wanawake, vijana na waendeshaji bodaboda, jambo ambalo limezua maswali kuhusu chanzo cha fedha hizo.
Hata hivyo, Naibu Rais alisema hataacha kuzuru nchi nzima kuwasaidia vijana na wanawake kiuchumi.
“Tuna tabia ya wanasiasa kuja na ahadi wakati wa kampeni. Tumeamua kuzingatia Mashinani kuwasaidia mama mboga na waendeshaji bodaboda. Wale wanaopinga mpango huu ni watu matajiri Nairobi. Wanataka tuache hili ili wapate cha kuahidi wakati wa kampeni, hapana, lazima tufanye sasa,” alisema.
Alisema mpango huo ni muhimu katika kubadilisha maeneo ya mashambani na kuharakisha maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika mkutano wa uwezeshaji wa kiuchumi kwa wafanyabiashara wadogo na waendeshaji bodaboda katika Soko la Kiawara, Nyeri Ijumaa, Naibu Rais alisema serikali inalenga kuinua wafanyabiashara na wakulima kwa kuingiza mtaji zaidi katika uchumi wa msingi.
“Mikakati tunayoifanya sasa ndiyo itakayosukuma uchumi wetu mbele. Lazima tuanze kwa kuboresha maeneo ya mashambani na kusaidia biashara ndogo ndogo na wakulima,” alisema.
Alifafanua kuwa serikali inajenga masoko 400 ya kisasa kote nchini kusaidia wafanyabiashara wasio rasmi, wengi wao wakifanya kazi katika maeneo ambayo hayana huduma za kutosha.
“Kwenye maeneo kama Kiawara, wakazi wengi ni wauzaji wa mboga. Masoko haya ya kisasa yatawapa hadhi na mahali salama pa kufanya biashara,” alisema.
Profesa Kindiki pia aliongeza kuwa serikali inapanga kuanzisha miradi ya makazi ya gharama nafuu katika miji , ambayo alisema itaunda ajira na kuboresha maisha vijijini.
Naibu Rais pia aliwahimiza vijana kutumia fursa za Mpango wa Fursa za Kitaifa kwa Vijana kuelekea Maendeleo (NYOTA), mpango wa serikali wa kuwawezesha vijana maskini kupitia mafunzo, msaada wa ujasiriamali, na upatikanaji wa ajira.
“Kupitia mpango huu, mtu anaweza kupata msaada wa kifedha wa takriban Sh50,000 na kuanzisha biashara,” alisema.
Naibu Rais alisema serikali ya Rais Ruto haitasumbuliwa na siasa za upande wowote.