Wazazi kulipia ada za mitihani ya kitaifa kuanzia mwaka ujao
KUANZIA mwaka ujao, wazazi watalazimika kulipia ada za mitihani kwa watoto wao, hatua inayomaliza rasmi msamaha wa ada uliokuwa ukifurahiwa na watahiniwa tangu ulipoanzishwa miaka kumi iliyopita.
Serikali itagharamia ada za mitihani kwa watahiniwa watakaotambuliwa kuwa wahitaji kupitia mpango wa utathamini wa hali ya maisha unaofanana na ule tata wa ufadhili wa elimu ya juu ulioanzishwa mwaka 2023.
Iwapo utatekelezwa, wazazi watalazimika kulipia gharama za mitihani ya Kenya Primary School Education Assessment (KPSEA), Kenya Junior School Education Assessment (KJSEA) na Kenya Certificate of Secondary Education (KCSE). Mitihani hii yote inasimamiwa na Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC).
Waziri wa Hazina ya Taifa na Mipango ya Kiuchumi John Mbadi aliambia Taifa Leo katika mahojiano maalum kuwa serikali itatumia mfumo wa ruzuku ya malengo ambao utawanufaisha tu wanafunzi ambao hawana uwezo wa kugharamia mitihani hiyo.
Hata hivyo, hakufafanua ni njia gani wanafunzi hao watatambuliwa.
“Wizara ya Elimu lazima ije na vigezo vya kuwatambua wanaoweza kulipa ada za mitihani. Kwa mfano, kama mtoto wako anasoma katika shule ya kibinafsi ambapo unalipa Sh300,000 kwa muhula au Sh1 milioni kwa mwaka, kwa kweli huwezi kulipa ada ya mtihani ya Sh5,000? Kwa nini ulazimishe walipa kodi—ambao baadhi yao hawana hata uwezo wa kujikimu—kugharamia mtihani wa mtoto wako?” alisema Bw Mbadi.
Msamaha wa ada ya mitihani ulianzishwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta mwaka 2015 kwa wanafunzi wa shule za umma, na mwaka 2017 ukafaidi shule za kibinafsi.
Msamaha huo ulilenga kuhakikisha wanafunzi wote wanafanya mitihani ya kitaifa na kuendeleza sera ya asilimia 100 ya uhamisho kutoka daraja moja hadi jingine.
Serikali ilitenga Sh4 bilioni kugharimia mitihani hiyo mwanzoni, lakini katika miaka miwili iliyopita imekuwa ikitenga Sh5 bilioni kila mwaka.
Wakati huo, watahiniwa wa mtihani wa KCPE waliokuwa wakilipa Sh800, huku wale wa KCSE wakilipa ada ya msingi ya Sh2,700 na Sh400 kwa kila somo.
Mpango huu mpya ni mabadiliko makubwa ya sera kutoka mfumo wa sasa wa msamaha wa ada kwa wote, unaowezesha wanafunzi wote katika shule za umma na kibinafsi kufanya mitihani bila gharama yoyote.
Bw Mbadi alisema uamuzi huo umechukuliwa kwa misingi ya uwajibikaji wa kifedha na usawa katika matumizi ya pesa za walipa kodi.
Alikanusha ripoti kuwa Hazina ya Taifa haijatenga fedha kwa mitihani mwaka huu.
Waziri alieleza kuwa bajeti ya mitihani ya kitaifa kwa mwaka huu ipo na Baraza la Mawaziri tayari limeidhinisha.
“Kutakuwa na utaratibu wa kutoa fedha hizo. Kwa hiyo, hakuna haja ya kuwa na wasiwasi. Wazazi wasikate tamaa,” alisema Bw Mbadi.
Aliongeza kuwa kuanzia mwaka ujao, wanafunzi wote hawatakuwa na uhakika wa kupata msaada wa serikali.
Katika miaka ya hivi karibuni, KNEC imekuwa ikikumbwa na changamoto za kifedha kulipa maafisa wanaohusishwa na mitihani kutokana na ongezeko la idadi ya watahiniwa tangu msamaha huo uanze.
“Lazima tuchunguze upya gharama hii na tujiulize, kwa nini tuwalipie ada ya mtihani wanafunzi wote, hata wale wa shule za kibinafsi? Tunapaswa kusaidia tu wale wasioweza kugharamia,” alisema Bw Mbadi.
Tangu mwaka 2015, serikali imekuwa ikigharamia mitihani ya KCPE, KCSE, na hivi majuzi tathmini mbalimbali chini ya mfumo mpya wa elimu (CBC), jambo lililosaidia kupunguza mzigo wa kifedha kwa familia wakati gharama ya maisha inaendelea kupanda.