Uncategorized

Cheo fiche cha Raila katika serikali ya Ruto

Na BENSON MATHEKA May 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MKUTANO wa Kiongozi wa ODM Raila Odinga na maseneta Alhimisi wiki hii na iliyotangulia ofisini kwake na mawaziri unamsawiri kama anayeshikilia cheo fiche katika Serikali Jumuishi ya chama chake na UDA cha Rais William Ruto.

Japo anasisitiza kuwa hayuko serikalini na makubaliano yake na Ruto ni ushirikiano uliokitwa katika azma ya kutuliza nchi, Bw Odinga anaonekana kuwa na ushawishi mkubwa ambao wachambuzi wa siasa wanasema unamsawiri kama rais mwenza katika utawala wa Kenya Kwanza.

Wanasema kutembelewa na maafisa wa ngazi ya juu serikalini wakiwemo mawaziri na makatibu kunaonyesha anatekeleza jukumu fulani fiche ambalo halijatangazwa.

“Kufikia sasa, na kwa kuzingatia anavyotembelewa na maafisa wakuu wa serikali na makubaliano yake na Rais Ruto, Raila anatekeleza jukumu la mshauri mkuu fiche wa kisiasa au msimamizi mkuu katika serikali,” asema mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Njoroge.

Anasema jinsi ilivyokuwa katika handisheki yake na Rais Uhuru Kenyatta katika utawala wa Jubilee, ndivyo inavyofanyika chini ya mpangilio wake na Rais Ruto ambapo maafisa wa serikali wanamtembelea kwa mashauriano.

“Si siri kwamba ushawishi wa Raila umeongezeka kwa kiasi kikubwa tangu aanze ukuruba wake na Rais Ruto.

Mawaziri, makatibu, mabalozi na wakuu wa mashirika ya umma sasa wanatembelea ofisi yake mara kwa mara kwa shughuli rasmi, ambazo anasema ni mashauriano.

Hii inaonyesha ana cheo fiche ndani ya utawala wa sasa kinachofanya maafisa hawa kumwendea,” asema Dkt Gichuki.Maafisa wa hivi majuzi kumtembelea katika ofisi yake ni pamoja na mawaziri Kipchumba Murkomen (Usalama wa Ndani), John Mbadi (Hazina ya Kitaifa), Hassan Joho (Madini), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika), Beatrice Askul (Jumuiya ya Afrika Mashariki), Opiyo Wandayi (Nishati), na Balozi wa China Guo Haiyan, miongoni mwa wengine.Katika kikao chake wiki hii na maseneta, Raila aliunga mkono hatua yao ya kutaka kurekebisha Katiba ili kukweza Seneti kuwa “Bunge Kuu” katika mfumo wa mabunge mawili wa Kenya.

Ziara ya seneti

Wakati wa ziara yake ya kipekee bungeni jana, Raila aliwakumbusha maseneta kuhusu historia ya mwaka 1963, wakati Seneti ya kwanza iliundwa kabla ya kuvunjwa na kurejeshwa tena kupitia Katiba ya 2010.

“Tunataka Seneti ifanye kazi ambapo maseneta watakuwa na mamlaka na majukumu. Lazima tuimarishe Seneti kama ilivyo Seneti ya Amerika,” alisema Raila.

Maseneta waliohudhuria kikao cha Alhamisi katika ukumbi wa Seneti, walifichua kuwa walimwalika Raila kutafuta msaada wake katika mpango wao wa kurekebisha Katiba, jambo ambalo wachanganuzi wanasema ni sawa na kutambua ushawishi wa cheo chake ndani ya serikali.

“Imekuwa heshima kwangu kujadili na @Senate_KE kuhusu suala muhimu la ugatuzi.

Tunajizatiti kurudi kwenye misingi ya mchakato huu wa mageuzi, tukishughulikia changamoto zilizopo ili kuhakikisha ugatuzi unatimiza ahadi yake ya awali na mwelekeo wake,” Raila alisema.

Spika wa Seneti Amason Kingi alisema alifurahi kushauriana na Bw Odinga.Mnamo Mei 16 katika ofisi yake ya Capitol Hill, Raila alikutana na Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen“Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa Onesmus Kipchumba Murkomen alinitembelea leo.

Waziri ni rafiki yangu wa miaka mingi,” alisema.

Mnamo Mei 19, alikutana na waziri wa Madini Ali Hassan Joho ambaye aliandamana na Makatibu Harry Kimtai (Madini), Betsy_Njagi (Uchumi wa Majini) na maafisa wengine wa wizara.Mchanganuzi wa siasa Abraham Otieno asema Raila ni zaidi ya mshirika katika serikali ya Kenya Kwanza.

“Ni nguzo ya utawala wa Ruto baada ya rais kutalikiana na aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua. Ana ushawishi mkubwa katika serikali hii ambao hata mawaziri hawawezi kuupuuza,” asema Otieno huku akiongeza kuwa mawaziri na makatibu wao hawawezi kushauriana na Bw Odinga bila baraka za Rais Ruto au iwapo hawatambui cheo au jukumu analotekeleza serikalini.

“Ni wazi kuwa akiwa nguzo muhimu katika serikali ya Kenya Kwanza, ana cheo au wadhifa ambao umefichwa na ndiyo sababu maafisa wakuu wa serikali wanashauriana naye,” asema.