Makatibu watatu wa wizara walia kupunguziwa bajeti
MAKATIBU Watatu katika Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda wameonya kuwa ajenda ya Rais William Ruto ya Mabadiliko ya Kiuchumi (Beta) chini ya wizara hiyo huenda ikakwama kufuatia kupunguzwa kwa bajeti ya Sh11.6 bilioni na Hazina ya Kitaifa.
Wabunge hao, Dkt Juma Mukhwana, Bw Hassan Abubakar (Uwekezaji) na Bi Regina Ombam (Biashara) – walifichua hayo walipofika mbele ya kamati ya Biashara, Viwanda na Ushirika ya Bunge la Kitaifa kuhusu mgao wao wa bajeti ya 2025/26.
Katibu Abubakar aliambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Ikolomani, Bernard Shinali kwamba Wizara yake ya imetengewa Sh2.13 bilioni kwa ajili ya maendeleo dhidi ya hitaji la Sh12.6 bilioni lililotolewa katika Taarifa ya Sera ya Bajeti ya 2025 (BPS) iliyoidhinishwa, na kuacha pengo la ufadhili la Sh10.5 bilioni.
“Hii itaathiri pakubwa utekelezaji wa miradi ya Beta na pia kuchelewesha kukamilika kwake,” Bw Abubakar aliambia kamati.
Hofu ya viongozi hao wakuu ilizua wasiwasi miongoni mwa wanakamati, ambao walikuwa wamehoji ni kwa nini miradi ya serikali inakwama licha ya kutengwa kwa bajeti.
Upungufu huo unaathiri Programu za Kukuza Uchumi (ESP) ambazo zinalenga kukuza uchumi wa nchi kwa kusaidia wafanyabiashara wadogo na kukuza ukuaji wa Biashara Ndogo, Ndogo (MSMEs) haswa katika sekta kama kilimo, miundombinu na biashara miongoni mwa mengine.
Dkt Mukhwana alifichua kuwa Idara yake ya Viwanda inakabiliwa na upungufu wa Sh610 milioni katika bajeti ya maendeleo.
Dkt Mukhwana alibainisha kuwa idara yake imetengewa Sh8.679 bilioni, ikiwa ni punguzo la Sh9.13 bilioni zilizokuwa zimependekezwa katika BPS.
“Upungufu huo utachelewesha miradi inayoendelea. Hii ni pamoja na mipango inayolenga uundaji wa nafasi za kazi, uongezaji thamani, na ukuaji wa uchumi,” alisema Dkt Mukhwana.
Katibu huyo pia alifichua kuwa kando na maabara za utafiti katika Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Viwanda nchini (KIRDI), Hifadhi za Kaunti na Viwanda (CAIPs) zitaathiriwa pakubwa na upungufu wa bajeti.
Bw Shinali na Makamu Mwenyekiti wake Marianne Kitany (Aldai) walitoa changamoto kwa serikali kumaliza miradi inayoendelea kabla ya kuzindua mpya.
“Ili kupata thamani ya pesa, ni lazima tukamilishe miradi iliyopo kwanza. Kuzindua miradi mipya kabla ya inayoendelea kukamilika wakati ambapo nchi inakabiliwa na matatizo ya kukusanya rasilimali ili kufadhili shughuli zake, si wazo zuri,” alisema Bw Shinali.
Bi Kitany alipendekeza kuwa serikali za kaunti na washirika wa kibinafsi waruhusiwe kufadhili na kusimamia CAIPs zao wenyewe.