Zubeida achaguliwa tena kuwa rais wa KEG
MWANAHABARI Zubeida Kananu amechaguliwa tena kuwa Rais wa Chama cha Wahariri Nchini.
Hii ni baada ya Bi Zubeida ambaye ni mtangazaji katika runinga ya KTN kupata kura 72 dhidi ya mpinzani wake Yvonne Okwara wa Citizen TV ambaye alipata kura 58 katika uchaguzi uliofanyika Jumamosi, Mei 24.
Francis Openda atakuwa naibu wa Bi Kananu.
Hapo awali, uchaguzi huo ulikuwa ufanyike Aprili 12, lakini uliahirishwa na kufanyika Mei 24.
Bi Okwara alituma pongezi zake kwa Bi Kananu akiwashukuru wanachama kwa kulinda demokrasia wakati wa uchaguzi.
“Hii imekuwa kampeni nzuri na nakubali matokeo na bado ninajivunia ujumbe tuliobeba – wa kuimarisha uaminifu, na madhumuni ya pamoja,” Okwara alisema.
Katika ujumbe mzito, Okwara alimpongeza mpinzani wake mkuu na wengine waliochaguliwa wakati wa uchaguzi huo.
“Kwa uongozi unaokuja: Natoa pongezi zangu za dhati. Mna kazi kubwa mbele yenu- kuunganisha chama na kurejesha imani katika taasisi yetu. Nawatakia kila la heri,” Bi Okwara alisema.
Wajumbe wengine waliochaguliwa wakati wa uchaguzi huo ni Agnes Mwangangi, Julius Bosire, Mildred Awuor, Linda Bach mwakilishi wa magazeti, huku Kenfrey Kiberenge akichaguliwa kama mwakilishi wa mtandaoni/kidijitali.
Wengine ni Ruth Nesoba, Martin Masai, na Mbugua Ng’ang’a.