Washirika wa Gachagua wataka muhuri wa serikali urejeshwe kwa ofisi ya AG
WASHIRIKA wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wametaka muhuri wa serikali urejeshwe katika afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wanadai kuwa muhuri huo ulihamishiwa katika ofisi ya Mkuu wa Utumishi wa Umma kinyume cha sheria na ulikuwa ukitumika kufanya miamala ya serikali kinyume cha sheria.
‘Katiba iko wazi kuhusu nani ndiye msimamizi wa muhuri wa serikali, nitazungumzia suala hilo Bungeni ili tufahamishwe iwapo muhuri huo unatumika kupiga mnada nchi yetu,’ alisema Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji.
Naye Naibu kiongozi wa Chama cha DCP) Cleophas Malala alidai kuwa muhuri huo unatumika kuchapisha fedha kwa ajili ya programu za ajira kwa vijana nchini.
‘Pesa hizo zinachapishwa kama ilivyokuwa 1992,’ alisema Bw Malala.
Bw Malala alisema Wakenya wanapaswa kuinuka na kuikomboa nchi kutoka kwa uongozi mbaya bila woga.
Kwa upande wake, Seneta wa Kiambu Karungo Wathang’wa alisema hali ni mbaya na akaahidi kumwandikia Spika wa Seneti kutaka kujua ni mikataba mingapi ya serikali imewekewa muhuri.
Mwakilishi wa Wanawake wa Kirinyaga Njeri Maina alisema kuwa lazima mhuri hiyo irejeshwe katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu.
‘Tulisikia kwamba muhuri wa umma umechukuliwa kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu, hatutaruhusu hili kutokea,’ alisema.
Alisema mamlaka ni ya Wakenya na wale ambao watatumia muhuri wa umma kwa njia isiyofaa watachukuliwa hatua.
Walimtaja Bw Gachagua kuwa mwanasiasa mkweli na kuapa kumlindwa dhidi ya aina yoyote ya unyanyasaji na Serikali.
Wakizungumza Ijumaa katika uwanja wa michezo wa Kairuri katika kaunti ya Embu wakati wa utoaji wa basari kwa wanafunzi wasiojiweza wa eneo bunge la Manyatta, viongozi hao walisema majaribio yoyote ya kumnasa Bw Gachagua yatakabiliwa na upinzani mkali.
Viongozi hao walionya kuwa Wakenya hawataruhusu serikali kumkamata na kumnyamazisha Bw Gachagua.
‘Ikiwa wewe ni mwanamume, jaribu kumkamata Gachagua na utajua Kenya inamilikiwa na akina nini,’ alisema Bw Malala.
“Tulisikia kuwa serikali ilitaka kumkamata Gachagua, serikali imeshindwa kutimiza wajibu wake na sasa inamlenga Gachagua,” akasema Bi Maina.
Bi Maina alilalamika kuwa Kenya Kwanza ilimtimua Gachagua serikalini kwa kuwaambia Wakenya ukweli.
“Hatutavumilia vitisho vinavyoelekezwa kwa Bw Gachagua,” akasema Bi Maina.
Naye Bw Mukunji, “Wametishia kumkamata Gachagua, acha wafanye hivyo, hatuwezi kuruhusu kuvurugwa kwa uchaguzi.”
Bw Wathang’wa alimtaja Gachagua kuwa kiongozi mzalendo na mwaminifu.
“Gachagua ndiye kiongozi wetu tunayemwamini na tutasimama naye,” akasema Bw Wathang’wa.
Viongozi hao waliikashifu serikali kwa kuwaondolea walinzi wabunge wanaokosoa uongozi wa Rais William Ruto.
Walionya kuwa iwapo lolote baya litatokea kwa wabunge hao, basi Dkt Ruto atawajibishwa.