Habari

Walimu wa shule za upili watoa notisi ya kugoma iwapo CBA itapuuzwa

Na WINNIE ATIENO May 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HUENDA walimu wa shule za upili wakaitisha mgomo muhula huu endapo Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) haitaandaa majadiliano kuhusu makubaliano ya nyongeza ya mishahara maarufu kama CBA kabla ya kusomwa kwa bajeti ya kitaifa mwezi ujao.

Walimu wanachama wa Muungano wa Walimu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (KUPPET) wamesema watalemaza shughuli za masomo iwapo TSC haitaongea nao ndani ya siku saba zijazo.

Mwenyekiti wa Kuppet Omboko Milemba na Naibu Katibu Mkuu Moses Nthurima wamesema ni lazima TSC iwaite kujadili nyongeza ya mshahara.

“Baada ya kila miaka minne, walimu huwa na mazungumzo na mwajiri wao na kutengeneza makubaliano mapya ya nyongeza ya mishahara na masuala mengine tata yanayowaathiri. Mwaka jana KUPPET iliwasilisha matakwa yao kwa mwaajiri, miezi ssaba imeisha bila mkutano kufanyika,” akasema Bw Milemba.

Mbunge huyo wa Emuhaya alisema mkutano huo unapaswa kufanyika kabla ya kupitishwa kwa bajeti mpya.

“Sababu nyongeza ya misharaha inafaa kuwekwa kwenye bajeti inayotarajiwa kusomwa mwezi ujao. Bunge la Kitaifa limeshaanza kutengeneza bajeti na hii ina maana ya kwamba walimu watakosa nyongeza ya mishahara kuwekwa kwenye bajeti itakayosomwa,” akaongoza.

Waziri wa Fedha Bw John Mbadi alisema huenda bajeti hiyo ikasomwa Juni 12.

Bw Nthurima alisema TSC iliwaahidi kwamba itawaita kwenye mkutano kujadili makubaliano ya nyongeza ya mshahara mwaka wa kifedha 2025/2026.

Wakiongea kwenye mkutano wa Kuppet huko Mtwapa, Kaunti ya Kilifi, Bw Nthurima alisema makubaliano ya nyongeza ya mishahara yanatarajiwa kufika kikomo mnamo Juni.

Wakuu wa Kuppet wamekuwa wakikutana Kilifi kwa siku mbili kujadili masuala ya muungano wao.

“TSC inajikokota sana, tuna wasiwasi kama muungano huenda bajeti ikasomwa bila ya kutilia maanani makubaliano yetu ya nyongeza ya mishahara. Tunatoa makataa ya siku saba kuitwa kwenye meza kujadili suala hili,” akasema Bw Nthurima.

Chama cha Walimu Nchini (KNUT) nacho kilikuwa kinatarajia kutia saini makubaliano ya nyongeza ya mishahara na TSC kabla ya kustaafu kwa aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji Nancy Macharia ambaye nafasi yake ishatangazwa.

Akiwaaga walimu wakuu wa shule za upili za umma mwezi uliopita, Bi Macharia aliwaambia mazungumzo kuhusu CBA hasa nyongeza ya mshahara yameanza.

Bi Macharia alisema wameweka mikakati kabambe kukabiliana na migomo ya mara kwa mara kwenye sekta ya elimu.

Matakwa ya Knut ni kuongezwa marupurupu, mishahara, uajiri wa walimu kukabiliana na uhaba mkubwa uliopo, walimu kuruhusiwa kuchukua likizo ya siku 90 kugombea viti vya kisiasa miongoni mwa masuala mengine.