Mauaji yaibua hofu ya kurejea kwa magenge yaliyokuwa yamenyamazishwa
MAUAJI ya wafanyabiashara wawili Nakuru Mashariki na Bahati wiki jana, kumeibua hofu wa kuchipuka kwa magenge hatari jijini Nakuru.
Wawili hao walipigwa risasi kwenye visa vya wizi wa mabavu, matukio ambayo yamesababisha wakazi waishi kwa hofu.
Katika kisa cha kwanza Jackson Mwangi, mfanyabiashara maarufu Nakuru Pipeline aliuawa na wezi waliojihami ambao walivamia duka lake karibu na Kanisa la Joyland mnamo Mei 21.
Bw Mwangi alikuwa na mkewe wakati ambapo wezi hao walivamia duka lake saa mbili usiku wakiwa na silaha hatari. Walitoweka na bidhaa yenye thamani ya Sh200,000.
Katika tukio jingine Paul Ndungu, mfanyabiashara Ndege, Kaunti Ndogo ya Bahati alipigwa risasi Ijumaa iliyopita usiku. Mvulana mwenye umri wa miaka minane naye aliaga dunia katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nakuru baada ya kupigwa na majangili.
Kamanda wa Polisi Nakuru Mashariki Samson Andanje alisema uchunguzi unaendelea na mauaji hayo yanafuatiliwa na maafisa kutoka Idara ya Upelelezi Nchini (DCI)
Kaimu Kamanda wa Polisi Lilies Wachira naye alisema polisi wameanzisha uchunguzi wa kuwanasa washukiwa.