Makala

Wivu wa kimapenzi uliosababishwa na shanga waletea mwanamke majeraha Samburu

Na GEOFFREY ONDIEKI May 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANAMKE moja anaendelea kuuguza majeraha mabaya kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Samburu jijini Maralal baada ya kupigwa na mume wa jirani yake kutokana na mzozo uliohusu kushonwa kwa shanga.

Salimo Priscilla Lolonyekie alikuwa amempa mwanamke jirani yake shanga akamilishe kuitengeneza lakini hakujua kufanya hivyo kungemvunia majeraha mabaya na nusura aonje mauti.

Mume wa jirani huyo Lempiris Lemargas alimtuhumu mkewe kwa kumtengenezea moran shanga hiyo lakini hali haikuwa hivyo.

Mkewe alipomwambia alipewa shanga hiyo aikamilishe na Bi Lolonyekie aliishia kuwa na fikira tofauti.

Alituhumu Bi Priscilla alikuwa akishirikiana na mkewe kuficha mapenzi aliyodai yalikuwa yamenoga kati yake na moran.

Hapo ndipo Lemargas alimvamia siku nne zilizopita na kumgonga kwa rungu akimwacha akiwa hana fahamu.

“Huwa silali na nikilala, bado mimi humsikia akinigonga kwa rungu mara si moja. Nilifikiria singeamka,” akasema Priscilla akiwa kwenye kitanda chake hospitalini.

Kichwa chake kimevimba, ushahidi tosha kuwa kando na kupigwa kwa rungu, pia aliangushiwa magumi mazito mazito.

Baada ya kumpiga Bi Priscilla, Lemargas alitoweka na bado anasakwa na maafisa wa usalama.

“Aligonga mlango wangu jioni hiyo. Nilifungua mlango, alinimulika kwa kurunzi machoni na singeweza kuona tena kisha akanipiga kwa rungu kichwani na akanivamia bila huruma,” akaongeza Bi Priscilla.

Nduguye Francis Lolonyekie alisema walimpata akiwa amepoteza fahamu, hapumui na wakamkimbiza hadi Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Baragoi.

Baadaye hali yake ilipokuwa ikiendelea kuwa mbaya ndipo alihamishwa, Hospitali ya Rufaa ya Samburu, Maralal na kuwekwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi.

Bw Francis alikashifu uvamizi huo akisema si wa kusamehewa huku akitaka maafisa wa usalama wamwaandame Lemargas ambaye alitoweka baada ya kutenda kosa hilo.

“Tulimpata amekosa fahamu na hata tulipambana sana kusaka fedha za kupata ambulensi ya kumsafirisha kutoka kijiji cha Serem Baragoi hadi Maralal,” akasema Bw Francis.

“Kile ambacho kinaniuma zaidi ni kwamba mshukiwa bado yupo huru naye dadangu akiendelea kuumwa. Tuliuza mali yetu kumpeleka hospitalini na haijakuwa rahisi,” akaongeza.

Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Samburu walithibitisha kuwa Priscilla aliumizwa kwenye fuvu la kichwa na damu ikavuja ndani kwa ndani ndiposa akapoteza fahamu.

“Lazima nisema ilikuwa bahati alinusurika. Tumeona dhuluma za kijinsia hapo awali lakini hii ilipita mpaka na ilikuwa katili kabisa. Kwa sasa yupo dhabiti,” akasema daktari moja hospitalini humo.

Kamanda wa Polisi wa Samburu Dickens Njogu alithibitisha tukio hilo na kusema polisi wanaendelea kumwaandama Lemargas. Bw Njogu alisema tukio hilo linasikitisha na akaomba umma uwasaidie kupata mshukiwa.

“Maafisa mshukiwa na tutamkamata. Hii haifai,” akasema Bw Njogu.

Wanaharakati na wananchi nao wamelalamikia kuongezeka kwa visa vya dhuluma za nyumbani kuanzia Serem hadi Baragoi, akisema vimechangiwa na washukiwa kutochukuliwa hatua zozote kwenye visa vya awali.