Omtatah sasa ataka polisi walioua 5 Angata Barikoi waadhibiwe
SENETA wa Busia Okiya Omtatah anataka maafisa wa polisi waliowaua watu watano wakati wa fujo kuhusu ardhi eneo la Angata Barikoi, Kaunti ya Narok wakamatwe na kushtakiwa.
Bw Omtatah ameitaka Kamati ya Seneti kuhusu Usalama, Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni, kuhusu mauaji ya raia hao waliokuwa wakipinga kile walichokitaja kama unyakuzi ardhi ya ekari 6,000 katika eneo hilo lililoko Trans Mara Kusini.
“Mnamo Aprili 28, 2025 watu watano, akiwemo mtoto mwenye umri wa miaka sita na mwalimu, waliuawa baada ya maafisa kutoka Wizara ya Ardhi kuanza kufanya usoroveya katika ardhi iliyoko sehemu ya Moyoi Trans Mara Kusini,” Seneta Omtatah.
“Nataka maelezo kuhusu kile kilichopelekea matumizi ya risasi yaliyochangia kuuawa kwa wakazi watano wa Ang’ata Barikoi na watu wengi wakajeruhiwa wakati wa maandamano kupinga shughuli hiyo ya usoroveya. Pia nataka maelezo kuhusu hatua ambazo zimechukuliwa kuhakikisha maafisa hao wanawajibikia makosa hayo,” akaeleza Seneta Omtatah.
Kiongozi huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha National Reconstruction Party (NPP) pia anasema majina ya wamiliki halisi wa ardhi ya Angata Barikoi watambuliwe na hatua zinazochukuliwa kusuluhisha mzozo wa ardhi wa muda mrefu katika eneo hilo ziwekwe wazi.
Bw Omtatah pia anataka kujua sababu zinazopelekea ardhi hiyo kufanyiwa usoroveya na kwa nini wakazi wanahitajika kuondoka.
Hii ni licha ya uwepo wa agizo la mahakama linalozuia kuchukuliwa kwa hatua kama hiyo hadi kesi hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa.
Aidha, Bw Omtatah anaitaka Kamati hiyo ya Seneti maelezo kuhusu ni nani aliyeamuru ardhi hiyo ifanyiwe usoroveya na ikiwa wakazi wa eneo hilo walishauriwa au kuhusishwa kwa njia yoyote.
Kamati hiyo ya Seneti inatarajiwa kutoa ripoti kuhusu uchunguzi ulioendeshwa na Mamlaka Huru ya Kufuatilia Utendakazi wa Polisi (IPOA) kuhusu kisa hicho.
“Vile vile, maelezo kuhusu hatua zilizochukuliwa kuhakikisha kuwa polisi waliohusika na mauaji hayo wanaadhibiwa kwa kuwafyatulia risasa raia wasio na silaha. Aidha, maelezo kuhusu hatua zinazochukuliwa kuwalipa fidia familia ambazo wapendwa wao waliuawa na kujeruhiwa katika kisa hicho na malipo ya gharama ya mazishi,” Bw Omtatah akaeleza.
Wiki chache zilizopita mzozo wa ardhi katika eneo la Angata Barikoi uligongwa vichwa vya habari kufuatia kuuawa kwa watu watano. Maafisa kadhaa pia walijeruhiwa katika purukshani hizo.
Miongoni mwa waliouawa ni mwalimu mmoja aliyedaiwa kupigwa risasi na afisa wa GSU wakati wa makabiliano ya kutaka kuzuia maafisa wa ardhi kuendesha usoroveya katika ardhi hiyo ya ukubwa wa ekari sita.
Watu watatu na familia 448 zinadai kumiliki ardhi hiyo, ambayo mvutano kuihusu ulianza miaka ya 1970s.
Taifa Leo iligundua kuwa kesi kuhusu mzozo wa umiliki wa ardhi hiyo imewasilishwa katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi, mjini Narok.