Wafanyabiashara, wasanii Nairobi wakemea matamshi ya Gachagua
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amekashifiwa na baadhi ya wafanyabiashara Nairobi waliodai kuwa analenga kuhujumu amani nchini kwa kuamsha makovu ya ghasia za uchaguzi tata wa 2007.
Wakiongea Jumatatu, Mei 26, 2025, wafanyabiashara hao kutoka Mlima Kenya walimtaka Bw Gachagua akome kuyatoa matamshi ya chuki na asubiri kutatua uhasama wake na Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2027.
“Heshima huwa ni njia mbili na wakati umefika ambapo lazima tuseme ukweli. Mbona unadanganya kuwa Bima Mpya ya Afya (SHA) haifanyi kazi? Umekuwa ukiwadharau wanasiasa wengine na kuendeleza matamshi ya kikabila,” akasema mmoja wa viongozi wa wafanyabiashara hao James Gichane.
Pia wafanyabiashara hao walikashifu Bw Gachagua kwa kuwachochea wanamuziki ambao walimtembelea Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki.
Walishangaa kwa nini Bw Gachagua alikerwa na mkutano huo ilhali Profesa Kindiki pia anatoka Mlima Kenya. Jumapili akiwa eneobunge la Othaya, Bw Gachagua aliwataka wafuasi wake wakatae muziki wa wanamuziki waliomtembelea Profesa Kindiki na pia kukwepa maeneo ya burudani ambako watakuwa wakisaka riziki.
Aliwataka wanamuziki hao waombe msamaha kutokana na ziara kwa Profesa Kindiki la sivyo watakuwa na kazi kubwa kuburudisha maeneo mbalimbali Mlima Kenya.
“Sisi tunaishi Nairobi na kutangamana na jamii nyingine wala huwezi kutuenezia siasa ya ukabila. Hata chama kipya ulichokibuni hakina haja ya kuwaunganisha Wakenya iwapo utaendelea kuongozwa na ukabila,” akasema Bw Karenjo.
Haya yanajiri wakati ambapo Muungano wa Wasanii na Waigizaji Mitandaoni Nchini (DCCAK) wametetea wanamuziki nchini na kusema kuwa wao si silaha ya kutumiwa na wanasiasa.
“Hata wasanii wanalindwa kikatiba wala Gachagua hafai kufikiria wao ni mali yake,” akasema Mwenyekiti wa DCCAK Bob Ndolo.