Habari za Kitaifa

Kindiki avua uprofesa, atoa makucha kwa Gachagua

Na CECIL ODONGO May 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki ametoa makucha yake kwa mtangulizi wake Rigathi Gachagua akimtaka amheshimu huku uhasama kati ya wanasiasa hao wawili Mlima Kenya ukiendelea kutokota.

Tukio la hivi punde ambalo limezua mgawanyiko kati ya wanasiasa hao wawili ni hatua ya Profesa Kindiki kukutana wasanii kutoka Mlima Kenya siku tatu zilizopita katika makazi yake mtaani Karen.

Bw Gachagua alidai kuwa wanamuziki waliomtembelea Profesa Kindiki ni wasaliti na wanastahili kuomba msamaha akitoa madai kuwa walilipwa Sh50,000 kama hongo.

Aidha alitoa wito kwa wakazi wa Mlima Kenya wasusia nyimbo na hafla za wasanii hao akisema wamekubali kutumia na utawala ambao hauzingatii maslahi ya eneo hilo lililomuunga mkono Rais William Ruto kwa dhati mnamo 2022.

Hata hivyo, Profesa Kindiki akizungumza Kaunti ya Kiambu wikendi alimkaba koo Bw Gachagua akimwonya asilete siasa za chuki ambazo zimepitwa na wakati kwenye uhasama wake na serikali.

“Kwako wakati ulikuwa kiongozi ulimpa hongo nani au kumpa mali yako? Kidogo ambacho tunapeana si eti kwa sababu tuna mali nyingi bali ni kutokana na roho nzuri,” akasema Profesa Kindiki.

“Tafadhali koma kutuzomea kwa sababu sisi si watoto wako. Usinipigie kelele na usilete siasa hizo za kale hapo eneo la Kati,” akaongeza akionekana mwenye hasira.

Tangu alipoteuliwa kuwa naibu rais, Profesa Kindiki amekuwa akionyesha uaminifu mkubwa kwa bosi wake huku akikwepa kukabiliana na Bw Gachagua moja kwa moja.

Mara si moja, Bw Gachagua amemrejelea kama mtu wa kusema ‘ndio, ndio’ kwa Rais Ruto wala hawezi kumpinga au kumkosea. Wandani wa Bw Gachagua pia wamekuwa wakimvamia Profesa Kindiki wakisema kazi yake ni uaminifu kwa Rais Ruto badala ya kupigania maslahi ya Mlima Kenya.

Kati ya wanamuziki watajika kutoka Mlima Kenya ambao walimtembelea Profesa Kindiki katika makazi yake ya Karen wiki jana ni Samidoh Muchoki, Karangu Muraya, Ben Githae, Jose Gaturura, DJ Fatxo, Sammy Irungu, Martin Wajanet na Ngaruiya Junior.

“Walipewa Sh50,000 na watu ambao wanaenda kuwaburudisha wamechoshwa na utawala huu ilhali hao ndio waliketi nao. Lazima tukome kuwafuatilia kwenye mitandao hadi pale watakapoomba msamaha kwa jamii,” akasema Bw Gachagua.

Aidha Profesa Kindiki ameonekana kuendeleza misururu ya mikutano Mlima Kenya, akionyesha ukakamavu zaidi hasa baada ya Bw Gachagua kuzindua chama chake cha DCP wiki mbili zilizopita.