Kitendawili kuhusu ‘utekaji nyara’ wa Koimburi polisi wakidai alighushi kunyakwa
HUKU utata ukigubika madai ya kutekwa nyara, kuteswa na kisha kuachiliwa kwa Mbunge wa Juja George Koimburi, wandani wake wamesema masaibu yake yalianza Ijumaa wiki jana.
Mbunge huyo alikuwa akisambaza hundi za basari katika Shule ya Msingi na Gachororo Ijumaa iliyopita, kulingana na wasaidizi wake.
Hapo ndipo ghafla bin vuu akatoweka kwa pikipiki, baada ya kulalamika kuwa alikuwa akiandamwa na watu alioamini kuwa maafisa wa usalama.
Wasaidizi wake waliwaambia wanahabari jana eneo la Juja kwamba sharti serikali ielezee kwa nini alikuwa akiandamwa na ndipo akaamua kukwepa kwa kutumia pikipiki.
Hata hivyo, washirika hao wa Bw Koimburi hawakutoa ushahidi kuonyesha akitoweka kukwepa kukamatwa.
Baadaye, Mbunge huyo alijitokeza Jumapili katika Kanisa la Full Gospel eneo la Mugutha, ambako watu wa familia yake wanadai alitekwa nyara na watu waliojifanya polisi. Walimweka ndani ya gari na kutoweka naye.
Kanda ya video iliibuka kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha watu nje ya kanisa hilo wakiwabembeleza raia waingilie kati kukimbiza gari hilo. Hata hivyo, video hiyo haijaonyesha wakati halisi ambapo Bw Koimburi alikamatwa na kurushwa ndani ya gari aina ya Subaru, jinsi familia yake ilidai.
Jana asubuhi, iliripotiwa kuwa mbunge huyo alipatikana akiwa amepoteza fahamu katika eneo la Kibichoi, kaunti ndogo ya Githunguri.
Hii ni baada ya Bw Koimburi kutoweka kwa saa kadhaa huku utata kuhusu kisa hicho ukiendelea kushamiri, polisi wakidai alighushi kutekwa kwake nyara “ili kukwepa kutiwa mbaroni kwake.”
Aidha, maafisa wa Usalama pia hawakutoa ushahidi kuhimili madai kwamba utekaji nyara huo ulikuwa feki.
Jana, mkewe Bw Koimburi, Anne, kupitia msaidizi wa mbunge huyo David Gatana, alisema mumewe alipatikana amepoteza fahamu katika shamba moja la kahawa na mhudumu wa bodaboda.
Wakisaidiana na wasamaria wema, walimpigia simu mkewe na wakamkimbiza katika Hospitali ya Karen, Nairobi kwa matibabu.
“Alituambia alidhulumiwa na polisi. Anang’ang’ana kuongea lakini ameshinda anahisi machungu zaidi,” Bw Gatana akaambia Taifa Leo.
Akiongea katika hospitali hiyo baada ya kumtembelea mbunge huyo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema Bw Koimburi alipigwa vibaya na yuko hali mbaya.
“Aliteswa na waliomteka nyara. Amepoteza sauti yake na madaktari wanafanya kila wawezalo kuhakikisha anaweza kuongea,” Bw Gachagua akasema.
Lakini msemaji wa polisi Michael Muchiri aliambia Taifa Leo kwamba serikali haikuhusika na madhila ya Bw Koimburi. Alieleza kuwa ikiwa alikuwa akisakwa angeagizwa kufika katika kituo cha karibu cha polisi au makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).
“Tumetathmini hali hiyo yote tangu Ijumaa Koimburi alipodai kukamatwa na maafisa wetu na hatimaye Jumapili alipodai tena kukamatwa. Katika hali hizo zote Koimburi akajaribu kuchochea hisia miongoni mwa wafuasi wake kwa sababu anasakwa kwa kisa cha ulaghai kuhusu ardhi katika eneo la Juja,” akasema Bw Muchiri.
“Aidha, anakabiliwa na kesi ambapo alijaribu kughushi stakabadhi zake za masomo na kuziwasilisha kama halali ili aidhinishwe kuwa ubunge wa Juja 2022,” akaongeza.