Habari za Kitaifa

Kindiki: Hii barabara ya Elwak Modogashe mliyokejeli itaisha kabla ya 2027

Na GITONGA MARETE May 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Rais Kithure Kindiki amewahakikishia wakazi wa Kaskazini mwa Kenya kwamba ujenzi wa barabara ya kilomita 750 kutoka Isiolo hadi Mandera utakamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Akizungumza alipotembelea mradi huo huko Kulamawe, Kaunti ya Isiolo siku ya Jumanne, Naibu Rais alisema mradi huo utakamilika kufikia Juni 2027.

Alisema juhudi za kufungua Kaskazini Mashariki mwa Kenya kwa maendeleo ya kiuchumi ziko kwenye mkondo sahihi huku serikali ikiharakisha ujenzi wa barabara hiyo kuu.

Kwa gharama ya Sh100 bilioni, mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Barabara Kuu ya Kenya (KeNHA) kwa kushirikiana na mashirika mengine ya serikali, ndio mradi mrefu zaidi wa barabara kuwahi kujengwa katika historia ya Kenya.

Jana asubuhi Naibu Rais alifanya ziara ya ghafla ya kukagua mradi huo  ukaguzi na akaahidi mradi huo wa kitaifa utakamilika kwa wakati.

“Kazi yangu ni kuhakikisha tunasonga mbele vizuri katika kutimiza ahadi hii. Nimezungumza na mwanakandarasi na jamii ya hapa na kuthibitisha kuwa kila kitu kinaendelea vizuri,” alisema.

Barabara hiyo imegawanywa katika sehemu 11 na inaanzia Isiolo kupitia Kula Mawe-Modogashe-Samatar-Wajir-Tarbaj-Kotulo-Kobo-Elwak-Garre-Rhamu hadi Mandera.

Alisema wanakandarasi saba wameteuliwa kutekeleza mradi huo.

Profesa Kindiki alitembelea sehemu mbili: Isiolo-Kulamawe na Kulamawe-Modogashe na akaahidi kurudi hivi karibuni kuangalia maendeleo ya sehemu nyingine.

“Barabara hii itasaidia katika kuimarisha usalama, kushughulikia ujambazi na ugaidi, na itachochea ukuaji wa kiuchumi katika eneo hili ambalo limekuwa likipuuzwa kwa muda mrefu,” alieleza.

Mradi  huo wa barabara unalenga kufungua eneo hilo kwa wawekezaji pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za serikali.

Utaunganisha Kaunti za Meru, Isiolo, Garissa, Wajir, na Mandera.

Katika ziara ya maendeleo ya hivi majuzi katika eneo hilo, Rais William Ruto aliwahakikishia wakazi kuwa atatekeleza mradi huo  alivyoahidi.

Naibu Rais alisema kuwa mashirika husika ya serikali yanashirikiana ili kusaidia wanakandarasi kufanya kazi kwa haraka.

“Vikosi vyetu vya usalama na maafisa wengine wa serikali wametumwa kuhakikisha uhusiano mzuri wa kazi kati ya wanakandarasi na wenyeji,” alisema Naibu Rais.