Habari

Serikali yamwadhibu Samidoh kwa kuimba wimbo wa ‘Wantam’

May 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KILE kilichoanza kama burudani ya kawaida kwa gwiji wa Mugithi, Samuel Muchoki almaarufu Samidoh, sasa kimegeuka kuwa mzozo wa kinidhamu unaotishia kazi yake ya polisi.

Masaibu yake yalianza Ijumaa, Mei 16, baada ya video yake akiwa kwenye tamasha moja la burudani kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Katika video hiyo, mashabiki wake wanaimba kwa sauti kauli ya kisiasa yenye ujumbe wa kumkosoa Rais William Ruto.

Mashabiki hao walikuwa wakiimba “Wantam” – kifupi cha “one term” (muhula mmoja) – kauli inayotumiwa na wapinzani wa kisiasa wa Rais Ruto katika kampeni za kumng’oa madarakani ifikapo 2027.

Kauli hiyo imepata umaarufu mkubwa kutokana na kampeni zinazoendeshwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye aliondolewa afisini na Bunge mwezi Oktoba 2024 baada ya kutofautiana na Rais Ruto.

Katika video hiyo, Samidoh – ambaye pia ni afisa wa polisi – anasikika akiwaongoza mashabiki huku wakiimba “Wantam” kwa msisimko mkubwa.

Video hiyo ilipowafikia maafisa wakuu wa Polisi katika makao makuu ya Huduma ya Polisi (NPS) Jogoo House, suala hilo lilijadiliwa kwa kina. Ifikapo Jumatatu, Mei 18, Samidoh alianza kuchukuliwa hatua.

Chanzo cha kuaminika kiliambia Taifa Leo kuwa maafisa wa ngazi za juu walikubaliana kumhamisha Samidoh kutoka makao makuu ya polisi mkoa wa kati hadi Kikosi cha Kukabiliana na Wizi wa Mifugo (ASTU) kilichoko Gilgil kama hatua ya kinidhamu.

Chanzo hicho kilieleza kuwa hatua hiyo ya kumhamisha Samidoh ni adhabu ya awali kutokana na video ya tamasha lake ambalo sasa linachukuliwa kama ukiukaji wa maadili ya afisa wa polisi.

Mwongozo wa Huduma ya Polisi unawazuia maafisa kushiriki shughuli zozote za kisiasa na wanatakiwa kudumisha kutopendelea upande wowote wa kisiasa huku wakiwa waaminifu kwa serikali iliyoko madarakani.

Afisa mmoja mkuu alisema baadhi ya makamanda walihisi kuwa Samidoh alikiuka Sheria za Utumishi (SSO) baada ya video hiyo kusambazwa

Mbali na kuhamishiwa ASTU, Samidoh pia anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi rasmi wa kinidhamu na wakuu wake.

Taifa Leo ilimtafuta Samidoh ili azungumzie kuhusu kuhamishwa kwake na ikiwa anakabiliwa na adhabu ya kinidhamu kutokana na sakata ya video ya “Wantam.”

Kupitia simu, alijibu kwa kifupi: “Nipo mahali siwezi kuzungumza kwa sasa. Tutaongea baadaye.” Simu zilizofuata hazikupokelewa.

Pia Taifa Leo ilijaribu kuwasiliana na Naibu Inspekta Jenerali wa polisi, Bw Gilbert Masengeli – ambaye ni mkuu wa Samidoh – lakini hakujibu simu wala ujumbe mfupi.

Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja pia hakujibu maswali ya Taifa Leo kuhusu suala hilo.

Kulingana na uzito wa tuhuma anakazokabiliwa nazo Samidoh, matokeo mbalimbali yanaweza kutolewa – yakiwemo kushushwa cheo, kutozwa faini, kupewa onyo, au hata kufutwa kazi.

Baada ya uchunguzi kukamilika, matokeo yatapelekwa kwa NPS ambapo Naibu Inspekta wa polisi  atayawasilisha kwa Inspekta Jenerali kwa uamuzi wa mwisho.

Samidoh alikuwa miongoni mwa wasanii zaidi ya 12 kutoka Mlima Kenya waliomtembelea Naibu Rais Kithure Kindiki nyumbani kwake Karen Ijumaa, Mei 23.

Katika mkutano huo, wasanii wa nyimbo za Injili na wa kidunia walijadiliana kuhusu namna serikali inaweza kusaidia sekta ya ubunifu.

Miongoni mwa waliokutana na Naibu Rais ni pamoja na Karangu Muraya, Ben Githae, Jose Gatutura, DJ Fatxo, Sammy Irungu, Martin Wajanet, na Ngaruiya Junior.

Hata hivyo, ziara hiyo imezua upinzani mkali kutoka kwa wakosoaji wa serikali kutoka Mlima Kenya wakiongozwa na Gachagua, ambaye aliwashambulia wasanii hao kwa madai ya “kuhujumu jamii ya Mlima Kenya.”

Aliwataka mashabiki wapuuze muziki wao na wamiliki wa vilabu kuacha kuwaalika.

Lakini Profesa Kindiki alitetea wasanii hao, akisema walikuwa wakitafuta msaada wa serikali kuvunja ukiritimba unaowafyoza katika sekta ya burudani.

Dennis Itumbi, Mkuu wa Miradi Maalum ya Rais na Mratibu wa Uchumi wa Ubunifu, alijibu mashambulizi ya Gachagua kwa kusema:
“Wasanii wa Kenya si kwaya yako binafsi, Bw Gachagua. Hauwezi kumiliki sauti zao, maamuzi yao wala imani zao,” alisema.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, sekta ya ubunifu ina idara maalum ya serikali, sera madhubuti, na mipango ya kuwawezesha wasanii kupata haki, kipato bora, na kuifanya sekta hii kuwa kitovu cha maendeleo ya kitaifa,” aliongeza Bw Itumbi.