23/07/2019

Buda akemea mke kugeuza binti yao kitega uchumi

Na DENNIS SINYO

Lurambi, Kakamega

Kalameni wa hapa alimkemea mkewe vikali akimlaumu kwa kumtumia binti yao ili kupokea hela kutoka kwa wanaume waliotaka kumchumbia.

Inasemekana kwamba mama huyo alikuwa na mazoea ya kuwakaribisha wanaume nyumbani mumewe akiwa kazini na kuhakikisha walikutana na binti yake mrembo ili awakamue pesa.

Penyenye zasema kuwa mama huyo alikuwa akipokea hela kutoka kwa wanaume hao kila mmoja akimtamani binti yake.

“Kila mwanaume aliyetamani kumchumbia demu huyo aliishia kutoa zaidi ya Sh5,000 ili kumshawishi mama huyo kumpa nafasi ya kuzungumza na binti yake. Mama alikuwa akiwachagua wanaume wenye pesa na kuwaalika kwake. Baadhi ya wanaume walikuwa wakirejea kwa mama huyo wakibeba shopping ya nguvu,” alisema mdokezi.

Baadhi ya majirani walionekana kutofurahishwa na tabia ya mama huyo na wakaamua kumpasha habari mumewe.

Jombi aliwaka kwa hasira aliposikia habari kwamba mkewe alikuwa amegeuza binti yake kuwa bidhaa ya kufanyia biashara. Jamaa alifika nyumbani na kumlaumu mkewe kwa kufurahia vinono kutoka kwa wanaume akiwaahidi binti yake.

“Badala ya kumuacha msichana ajitafutie mwanaume ?anayempenda, wewe unakaribisha hapa wanaume wa kila aina haja yako ikiwa pesa tu,’’ aliteta jamaa.

Jamaa na mkewe waligombana kwa muda hadi mama akakiri?makosa.

“Unafurahia tu kutafuna mali ya wenyewe bila kujua wengi wao wanajua sheria na huenda wakakuchukulia hatua msichana akiolewa kwingine,’’ alisema jamaa.

Mama huyo aliomba msamaha na kuahidi kutowakaribisha wanaume tena nyumbani. Alidai hata binti yao alikuwa amewakataa wanaume hao.

Binti yake alifurahia hatua hiyo na kusema alikuwa amechoshwa na tabia ya mama yake.