Habari za Kitaifa

Polisi wameua raia 136 ndani ya mwaka mmoja uliopita – IPOA

Na JUSTUS OCHIENG’ June 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAMLAKA ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA)-asasi yenye jukumu la kuzuia visa vya ukiukaji wa sheria miongoni mwa polisi- imekabiliwa na wakati mgumu kuhakikisha polisi wanaokiuka sheria wanawajibikia makosa yao.

Kulingana na mwenyekiti wa IPOA Isaack Hassan, asasi hiyo imepokea na kushughulikia jumla ya malalamishi 33, 791 na wamekamilisha kuchunguza malalamishi 6, 082 tangu asasi hiyo ilipobuniwa.

Lakini anasema, ndani ya mwaka mmoja uliopita, jumla ya vifo 136 vya raia vimehusishwa na maafisa wa polisi.

Isitoshe, watu wengine 59 wameripotiwa kufa ndani ya vizuizi vya polisi, wa hivi punde akiwa mwalimu na bloga Albert Ojwang’.

Kutokana na uchunguzi wake, IPOA imefaulu kufikisha jumla ya kesi 268 mahakamani.

Takwimu hizi za kuogofya zinatoa taaswira ya taifa ambalo limezongwa na utamaduni wa mapuuza ya sheria miongoni mwa maafisa wa usalama, hali inayoonyesha kuwa nchi hii inayo rekodi mbaya katika udumishaji wa haki za kibinadamu.

Bw Hassan anasema, kando na kuchunguza visa vya maafisa wa polisi kukiuka sheria, IPOA pia huendesha ukaguzi katika vituo vya polisi kubaini ikiwa ni faafu wa utekelezaji wa majukumu ya maafisa hao.

Mwenyekiti huyo alisema mamlaka hiyo pia imechunguza visa vya ukiukaji sheria polisi wanapokabiliana na waandamanaji.

“Kutokana na vifo 60 vilivyotokana na maandamano vilivyosajiliwa na IPOA, mamlaka hiyo imekamilisha kuchunguza visa 22. Aidha, inafuatiliwa visa 36 na imefikisha visa viwili sasa kortini.” Bw Hassan akasema.

Alisema IPOA pia imerekodi visa 233 vya majeruhi nyakati za maandamano ambapo visa 191 vinachunguzwa wakati huu.

“Kati ya visa vilivyosalia, uchunguzi kuhusu visa 42 ulisitishwa huku visa viwili vikipitishwa kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP),” Bw Hassan akasema.

Kuhusu visa vya utekaji nyara na mauaji ya kiholela yanayohusiana na polisi ambayo IPOA imepokea ndani ya miezi 12 iliyopita, Bw Hassan alisema wamepokea jumla ya malalamishi 4, 170 na kufikisha jumla ya uchunguzi kuwa 889.

“IPOA imesajili visa 49 vya watu kutoweka kwa njia ya kutatanisha, visa 136 vya mauaji yanayohusu maafisa wa polisi na visa 59 vya vifo katika vizuizi vya polisi,” Bw Hassan akasema.

Kuhusu idadi ya maafisa wa polisi ambao wameshtakiwa au kuadhibiwa kutokana na uchunguzi wa IPOA ndani ya mwaka mmoja uliopita, Bw Hassan alisema ni maafisa 11 walishtakiwa ndani ya 2024.

“Kesi zingine 268 dhidi ya maafisa wa polisi waliokiuka sheria kazini vingali katika mahakama mbalimbali. Kesi 82 kati ya hizo zinatokana na uchunguzi ulioendeshwa 2024 ilhali kesi 10 zinatokana na uchunguzi uliofanywa 2025,” akaongeza.

Hata hivyo, mwenyeketi huyo hakuchelea kuweka wazi kuwa IPOA inakumbwa na changamoto si haba katika utendakazi wake.

“Baadhi ya changamoto hizo ni; mgao finyu wa bajeti, ukosefu wa idadi ya kutosha ya maafisa wa uchunguzi kwani wakati huu tuko na wachunguzi 77 pekee ilhali tunahitaji jumla ya wachunguzi 404,” akasema.