Madiwani wadai kutishiwa maisha baada ya kuwasilisha hoja ya kutimua Gavana Guyo
MADIWANI wa Bunge la Kaunti ya Isiolo sasa wanadai maisha yao yako hatarini baada ya kuwasilisha hoja ya kumtimua Gavana Abdi Guyo.
Jumanne iliyopita, madiwani hao walizima simu zao na kuenda mafichoni baada tu kuwasilishwa kwa notisi ya kumtimua Bw Guyo. Wakati huo usalama ulikuwa umeimarishwa mno kwenye Bunge hilo la kaunti.
Aidha Bunge la Kaunti limeratibu mikutano ya ushirikishaji wa umma Jumatano kwenye wadi zote 10 huku mjadala kuhusu hoja ya kumtimua gavana ikijadiliwa na kupigiwa kura Ijumaa.
Wakazi pia wametakiwa wawasilishe maoni yao kwa Karani wa Bunge la Kaunti kupitia baruapepe ya kaunti.
Tangu kuwasilisha hoja hiyo, madiwani hao wamekuwa mafichoni huku wakidaiwa kuwahepa baadhi ya watu wenye lengo la kuwatishia ili waondoe hoja hiyo. Pia wamejificha wakijali usalama wao.
Ijumaa wiki jana madiwani 16 kati ya 18 waliandaa kikao na wanahabari wakidai wametishiwa maisha. Spika Mohamed Roba alielekezea lawama kwa wakuu wa kaunti kwa kuwatishia na kuwahangaisha madiwani.
Diwani wa Burat Nicholas Lorot alisimulia jinsi ambavyo walifuatiliwa na watu waliowashuku wakitoka Nakuru hadi Machakos
“Tulifuatwa na watu waliokuwa wamejihami vikali kuanzia saa tisa asubuhi hadi tulipofika tulikokuwa tukienda. Mmoja wa wafuasi wetu alitekwa nyara, akapigwa kisha kutupwa kwenye kichaka. Hatutatishwa tunapotekeleza majukumu yetu ya kikatiba,” akasema Bw Lorot.
Ingawa madiwani wote 18 mwanzoni walikuwa wakiunga mkono hoja hiyo, wawili wamebadilika na sasa wanaegemea mrengo wa Bw Guyo.
“Kuna uongozi mbaya na uhalifu ambao unaendelea hapa Isiolo na pia tunakashifu kuendelea kupanda kwa taharuki ya kisiasa huku tukitoa wito kwa viongozi wawe kielelezo bora,” akasema Bw Roba.
Diwani wa Ngaremara Peter Losu aliongeza kuwa watachukua tahadhari wakisafiri hadi Isiolo mnamo Jumatano.
“Tumeandikisha taarifa na polisi na tuna matumaini hatua itachukuliwa hivi karibuni. Hata hali iwe vipi bado tutatekeleza majukumu yetu ya kikatiba bila kuuziwa uoga au kuhangaishwa,” akasema.
Gavana Guyo anakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya afisi, kukiuka sheria za uongozi wa kaunti na kuendelea kuongezeka kwa deni la kaunti kupitia matumizi mabaya ya fedha.
Pia anadaiwa kuyatoa matamshi yasiyo ya heshima na ya kimadharua dhidi ya Seneta wa Isiolo Fatuma Dullo.