Habari za Kitaifa

Tutasuka Pentagon itakayompa Ruto ‘TuTam’, wandani wa serikali wasema

Na DOMNIC OMBOK July 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANDANI wa Rais William Ruto wameashiria kuwa watafufua Muungano wa Pentagon ambao ulikuwa maarufu katika ODM mnamo 2007 kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Mnamo 2007, ODM ilibuni muungano huo ambao uliwashirikisha Rais Ruto, Kinara wa Upinzani Raila Odinga, Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi, waliokuwa mawaziri Najib Balala, Charity Ngilu na marehemu Joe Nyaga.

Pentagon ilitekeleza wajibu muhimu kuhakikisha ODM inawika kwenye kura hiyo ambayo Bw Odinga amekuwa akisisitiza aliishinda lakini akapokonywa ‘tonge mdomoni’

Waziri wa Afya Aden Duale alisema kuwa serikali ya sasa inachapa kazi na ina marafiki maeneo yote nchini kwa hivyo watabuni muungano sawa na huo wa Pentagon.

“Wale ambao walikwepo 2007 wamejikusanya sana na ni msingi wa utawala huu. Tutafufua Pentagon,” akasema Bw Duale akishangiliwa na umati jijini Kisumu.

Msaidizi wa Rais, Farouk Kibet alisema kuwa siasa za urithi ambazo zinapangwa kwa sasa huenda zikafaa eneo la Nyanza ambalo kwa sasa linaunga Serikali Jumuishi.

“Tuendelee na umoja na baada ya Rais Ruto kumaliza hatamu yake, uongozi mwingine utatoka Nyanza,” akasema Bw Kibet.

Wakati wa hafla hiyo ya kuchangishia Bunge la Wananchi Kisumu, Bw Duale na viongozi wengine walishutumu upinzani kutokana na ghasia ambazo zilitokea mnamo Juni 25 ambapo zaidi ya watu 15 walifariki kwenye maandamano ya kitaifa.

Viongozi wa wanaogemea mrengo wa serikali waliwarejelea viongozi wa upinzani kama wachochezi ambao wanajificha nyuma ya maandamano ya Gen Z kuendeleza ghasia na uharibifu wa mali.

“Naweza kuandika kitabu kuhusu Justin Muturi, Rigathi Gachagua, Fred Matiang na wandani wao. Wakati wa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, waliwaua Waislamu wengi,” akaongeza Bw Duale.

Waziri huyo alimrejelea aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangí kwa kushuhudia kile ambacho alikisema ni mauaji yaliyoidhinishwa na serikali.

“Matiang’i ndiye mwasisi wa mauaji ya kiholela. Kulikuwa na makontena ya miili Nairobi, Mto Yala na Mto Tana,” akasema Bw Duale.

Mbunge wa Kikuyu na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah alishutumu upinzani akisema kuwa siasa zao zinaegemea mkondo wa kikabila.

“Hawa ni wapangaji ghasia na kile tulichoona wiki jana kilikuwa cha kuondoa serikali mamlakani. Sisi si binamu, sote ni ndugu na dada,” akasema Bw Ichung’wah akionekana kumlenga sana Bw Gachagua.

Alipokuwa akihutubu Ijumaa wiki jana, Dkt Matiangi alionekana kuchoshwa na madai kuwa aliratibu mauaji ya kiholela kwenye utawala uliopita.

Badala yake, alitoa wito wa uchunguzi ufanywe kuanzia pale Kenya ilipata uhuru mnamo 1963, akisema yupo tayari kumwaga mtama kuhusu kilichotokea kwenye serikali iliyopita.