Mbadi akanusha madai mkewe anataka ubunge Suba Kusini 2027
WAZIRI wa Fedha John Mbadi ameanza kukabiliwa na maasi eneobunge la Suba Kusini baadhi ya wanasiasa wakimshutumu kwa kumpendekeza mkewe Rhoda awanie kiti hicho cha ubunge mnamo 2027.
Bw Mbadi awali alikuwa amesema angepambana na Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi 2027 kabla ya kubadilisha nia hiyo baada ya kuteuliwa kwenye baraza la mawaziri.
Bi Rhoda amekuwa akimwakilisha mumewe kwenye hafla za mazishi na mikutano mingine ya umma kwenye eneobunge hilo.
Bw Mbadi amekuwa akijitetea kuwa wizara yake ina majukumu mengi ndiposa amekuwa akimtuma mkewe katika hafla za mazishi na umma Suba Kusini.
“Mimi huzungumza mara kwa mara na Rais William Ruto pamoja na maafisa wa ngazi ya juu serikalini. Siwezi kupata muda wa kutosha wa kuwa na wakazi wa eneobunge letu,” akasema Bw Mbadi.
“Tunafanya kazi za kijamii pamoja na Nyasembo (Rhoda) na kumtuma aniwakilishe haimanishi kuwa sasa anataka ubunge. Mimi si mtu ambaye hutaka wanafamilia wake wakwamilie mamlaka,” akaongeza.
Hata hivyo, alisema kuwa atakuwa na ushawishi kuhusu nani atakuwa mbunge wa eneo hilo 2027 kutokana uzito wa wadhifa ambao anaushikilia serikalini.
“Sina Hazina ya Kustawisha Maeneobunge (CDF) lakini nina mamlaka ya kalamu kupitia rais. Yeyote ambaye anataka kuwa mbunge ashirikiane nami kwa sababu nafuatilia jinsi ambavyo serikali inatumia kuhusu miradi mbalimbali,” akasema Bw Mbadi.
Waziri huyo alisema kuwa atatoa mwelekeo wake wa kisiasa wakati muafaka ukifika huku akisema alichukua mapumziko kutoka kwa siasa baada ya kuteuliwa waziri.
Wakati huo huo waziri huyo alisema anafanya juu chini kuhakikisha kuwa miradi ya miundomsingi inafaulu. Alisema ametenga pesa za kutosha kufadhili miradi hiyo.
Katika eneobunge lake alisema pesa zimetengwa za kumaliza barabara ya Sindo-Magunga-Sori na mwanakandarasi amepewa jukumu la kumaliza kazi hiyo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.