Gachagua aonywa anaweza kushtakiwa ikibainika alihusika na ghasia za maandamano
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua atakamatwa na kushtakiwa kama Mkenya mwengine yeyote iwapo ushahidi utamhusisha na ghasia zilizoshuhudiwa nchini mnamo Juni 25, Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) ilisema Jumatatu.
Mkuu wa DCI Mohamed Amin alisema kuwa hakuna mwanasiasa ambaye ana kinga cha kukamatwa nchini serikali inapoendelea kuwalenga waliofadhili maandamano hayo ya wiki jana.
Ghasia, mauaji na uharibifu wa mali ulishuhudiwa wakati wa maandamano hayo yaliyokuwa ya kuadhimisha mwaka moja tangu Gen Z wavamie Bunge la Kitaifa mnamo Juni 25, 2024.
“Kuhusiana na Rigathi, ningependa kuweka mambo bayana kuwa hana kinga yoyote ya kutoshtakiwa. Yeye ni kama Mkenya mwengine ambaye yuko chini ya sheria za nchi,” akasema Bw Amin.
“Iwapo uchunguzi wetu utabaini alikuwa akihusika na kupanga ghasia, fujo na uharibifu uliotokea, basi sheria itachukua mkondo wake dhidi yake,” akaongeza.
Bw Amin alikuwa akiongea wakati ambapo alikuwa akieleza taifa kuhusu mahali ambapo uchunguzi umefikia kuhusu matukio ya Jumatano iliyopita yaliyotikisa nchi,
Takwimu zilizotolewa na serikali kupitia Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen zilisema watu 10 walifariki katika maandamano hayo.
Hata hivyo, mashirika ya kijamii kama Shirika la Amnesty limeweka idadi hiyo kuwa watu 16.
Mkuu huyo wa DCI alifichua kuwa kufikia sasa, uchunguzi wao umeonyesha kuwa ghasia hizo kwenye maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Nairobi, zilikuwa zimepangwa.
“Uchunguzi wetu umeonyesha matukio ya kushtua. Kumekuwa na uharibifu wa miundomsingi ya serikali, bunduki kadhaa zikaibwa na vifaa vya polisi vikapotea na baadhi ya silaha zimetumika kwenye wizi,” akasema Bw Amin.
“Matukio haya yanaonyesha kuwa ghasia hizi zilipangwa na tunawaendea waliopanga na kufadhili fujo hizi. Watawajibikia vitendo vyao hivi karibuni,” akasema.
Bw Gachagua baada ya maafa yaliyotokea Juni 25, mnamo Alhamisi wiki jana alishutumu serikali kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.
Bw Amin aliwataka walioathirika na ghasia hizo wajitokeze, hasa wale ambao maduka yao yalivunjwa na kuporwa ili kusaidia kwenye uchunguzi.
Kufikia Juni 30, DCI ilithibitisha kuwa Wakenya 485 walikuwa wamenyakwa, 448 wakashtakiwa na wengine 37 bado wanachunguzwa.