Uingereza yajibu Murkomen kuhusu maandamano nchini
UINGEREZA haikuingilia masuala ya ndani ya Kenya kwa kutaka waandamanaji walindwe na polisi, Naibu Balozi wa nchi hiyo nchini amesema.
Akijibu madai ya serikali ya Kenya kupitia Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kwamba Uingereza ilishirikiana na mabalozi wengine wa kigeni kuingilia masuala ya ndani ya nchi, kwa kutaka waandamanaji walindwe kabla ya maandamano yaliyofanyika Juni 25, Naibu Balozi wa Uingereza nchini Kenya, Dkt Ed Barnett, alisema walifanya hivyo kwa nia njema.
Akizungumza katika mahojiano na kipindi cha Fixing the Nation cha runinga ya NTV, Dkt Barnett, alitetea taarifa ya pamoja iliyotolewa na mabalozi wa mataifa ya kigeni, akisisitiza ilitolewa kuhimiza maandamano ya amani na kutetea haki za binadamu.
Kwa mujibu wa Dkt Barnett, taarifa kama hizo ni sehemu ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Kenya na Uingereza, ambao unahusisha mazungumzo ya wazi, hata kuhusu masuala magumu.
Alieleza kuwa Uingereza huwa inashiriki mazungumzo ya wazi na ya faragha na Kenya kuhusu masuala kama vile haki za binadamu na utawala bora.
“Kwa kuwa sisi ni washirika wa karibu wa Kenya, sehemu ya uhusiano wetu ni kufanya mazungumzo magumu na rafiki wa karibu. Baadhi ya mazungumzo hayo hufanyika kwa faragha, na mengine,panapohitajika, hutangazwa hadharani,” alisema Barnett.
Dkt Barnett alisisitiza kuwa kuwawajibisha wote waliokiuka sheria, bila kujali mrengo wanaotoka ni muhimu katika kupunguza mvutano na kuzuia fujo zaidi.
“Yeyote aliyekiuka sheria anapaswa kuwajibishwa. Hili ni muhimu ili kupunguza mvutano na hatari ya ghasia zaidi,” aliongeza.
Akizungumza na wanahabari katika Harambee House jijini Nairobi Alhamisi iliyopita, Murkomen, kwa hasira, alikashifu jamii ya kimataifa kwa kuingilia siasa za Kenya bila kufanya uchunguzi wa kina.
Katibu wa wizara hiyo, Dkt Korir Sing’oei, pia alipuuza mabalozo hao kwa msimamo wao kuhusu maandamano.
“Asanteni kwa taarifa yenu. Maandamano ya kidemokrasia yanapaswa kulindwa, lakini juhudi zozote za kuyatumia maandamano hayo kwa malengo ya kuvuka mipaka ya katiba haikubaliki,” alisema.