Ripoti: Mauaji yamesukuma raia kufyata ndimi zao, kujikunyata kwa woga
WAKENYA wamefumbwa vinywa huku wakinyimwa uhuru wa kujieleza, kutekwa nyara, kuuawa kiholela, kuandamwa mitandaoni huku wanahabari wakidhulumiwa na maafisa wa serikali, kinyume cha Katiba.
Hii ni kulingana na ripoti mpya iliyotolewa na shirika la Civicus, linalofuatilia tishio kwa mashirika ya kijamii kote ulimwenguni katika majukwaa mbalimbali mitandaoni.
Kulingana na shirika hilo inaloshirikisha mashirika mbalimbali ya kijamii ulimwenguni, Kenya iko katika kundi la pili la mataifa ambayo raia wanadhibitiwa na kudhulumiwa na serikali zao.
Ripoti ya hivi punde kuhusu Kenya yenye kichwa, “Polisi Bullets, Digital Chains: State-Sanctioned Brutality in Kenya’s Peaceful Youth-Led Uprising” ilitolewa Juni mwaka huu wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja tangu maandamano ya 2024.
Ripoti hiyo inaelezea hatua zilizochukuliwa na serikali kunyamazisha raia kupitia vitendo vinavyohujumu haki zao za kimsingi.
“Serikali ya Kenya Kwanza ilichukua hatua dhidi ya waandamanaji kupitia matumizi ya nguvu kupita kiasi na kupelekea vifo vya watu wengi na mamia ya wengine wakiwa hawajulikani waliko. Tangu wakati huo, imeendelea kudhibiti nafasi ya watu kujieleza kwa njia huru, kupitia maandamano ya amani na kukosoa serikali mitandaoni,” akasema Katibu Mkuu wa Civicus Mandeep Tiwana.
“Juhudi hizi za serikali za muda wa mwaka mmoja zilionyesha jinsi maafisa wa usalama nchini Kenya wanatumia mbinu za kikoloni ambazo hazisaidii umma. Wanawanyazisha watu wanaoitisha haki na uwajibikaji,” ripoti hiyo inaongeza.
Maandamano ya vijana wa Gen Z yalilipuka mnamo Juni 2024 kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 uliopania kuongeza ushuru katika mazingira ya kudorora kwa uchumi.
Baadaye, maandamano hayo yaligeuka majukwaa ya kulaani utepetevu wa serikali, ukatili wa polisi, ubadhirifu na ufisadi miongoni mwa maafisa wakuu wa serikali.
Kilele cha maandamano hayo kilishuhudiwa mnamo Juni 25, 2024 waandamanaji walipovamia majengo ya Bunge.Serikali ilijibu kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji wakati na baada ya maandamano hayo.
Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNCHR) iliripoti kuwa, angalau watu 60 walikuwa wameuawa kutokana na machafuko hayo kufikia Oktoba 31 na jumla ya watu 82 walikuwa hawajulikani waliko kufikia Desemba 26, 2024.
Baadaye, maiti nyingi zilipatikana ndani ya misitu, mito, matimbo ya mawe na hifadhi za maiti; baadhi ya maiti hizo zikiwa na alama za kuonyesha watu hao waliteswa kabla ya kuuawa.
“Watawala wamevuruga mawasiliano kupitia intaneti nyakati za maandamano, wametoa onyo kwa kampuni za kuendesha mitandao hiyo, kuifungulia mashtaka au kuizima,” ripoti hiyo inaeleza.
Wabunge pia waliwasilisha mswada unaolenga kuwafuatilia watumiaji intaneti, na kuipa serikali mamlaka makuu yasiyodhibitiwa.
Wabunge pia walipendekeza nyongeza ya magao wa bajeti kwa polisi kuwawezesha kufuatilia shughuli za Wakenya mitandaoni.
Mapendekezo hayo mawili bado yanashughulikiwa katika Bunge la Kitaifa. Wakati huo huo, polisi wamekuwa wakiwaandama wanaharakati mitandaoni moja kwa moja.
Mnamo Mei 2025, mwanablogu Rose Njeri alikamatwa kwa kuunda jukwaa la kuwawezesha Wakenya kutuma maoni yao bungeni kuhusu Mswada wa Fedha wa 2025.
Alizuiliwa kwa saa 90 kabla ya kufikishwa kortini na kushtakiwa kwa kosa la kukiuka Sheria kuhusu Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Kimtandao.