Raia kuzuiwa kuandamana Bunge, majengo ya serikali mswada wa Passaris ukipita
UTATOZWA faini ya hadi Sh100,000 au kifungo cha hadi miezi mitatu jela iwapo utapatikana na hatia ya kushiriki maandamano katika maeneo yasiyoruhusiwa, ikiwa Mswada ulio bungeni utapitishwa kuwa sheria.
Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mpangilio wa Umma, 2025, uliodhaminiwa na Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Nairobi, Bi Esther Passaris, unapendekeza kutengwa kwa maeneo matatu ambayo waandamanaji hawataruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara au maandamano.
Kulingana na mswada huo, maeneo hayo ni: ndani ya mita 100 kutoka majengo ya bunge, maeneo yanayolindwa (kama Ikulu) na majengo ya mahakama.
Iwapo mswada huo utakuwa sheria, Waziri wa Usalama wa Ndani kwa ushauriano na serikali ya kaunti, ataweza kuteua maeneo maalum katika miji mikuu ambako maandamano yatafanyika.
Hii ina maana kwamba waandamanaji watatakiwa kukusanyika katika maeneo hayo maalum tu, na ikiwa wana malalamishi, viongozi wao ndio watakaokutana nao kuwasikiliza.
Mswada huo unaeleza kuwa yeyote atakayekiuka masharti hayo atakuwa ametenda kosa la jinai na akipatikana na hatia atatozwa faini isiyozidi Sh100,000 au kifungo kisichozidi miezi mitatu au adhabu zote mbili.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wameanza kuonyesha wasiwasi kuhusu mswada huo, wakisema ni mgumu kutekelezeka kwa hali halisi nchini Kenya.
Mbunge wa Nyakach, Bw Aduma Owuor, alisema sheria hiyo haitatatua matatizo ya msingi ya waandamanaji, naye Mbunge wa Kisumu Magharibi, Bi Rosa Buyu, alisema kupangiwa eneo maalum la kuandamana kunapunguza nguvu ya maandamano.
Wakili wa Masuala ya Katiba, Bw Bob Mkangi, alisema mswada huo unakiuka Kifungu cha 37 cha Katiba kwa kuwa unadhibiti uhuru wa kujieleza.
Alisema kiini cha maandamano ni kuvuruga hali ya kawaida ili kushinikiza wanaotawala kusikia kilio cha wananchi.
Wakati huohuo, baadhi ya wabunge kama Bw Abdirahman Mohamed wa Mandera Mashariki na Bw Francis Sigei wa Sotik, waliunga mkono mswada huo wakisema ni hatua ya kuhakikisha usalama na utulivu wa taifa.