Habari

Pigo kwa Kihika korti ikiruhusu ombi linalotaka atimuliwe mamlakani liendelee kusikizwa

Na JOSEPH OPENDA July 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JUHUDI za Gavana wa Nakuru Susan Kihika za kuzuia kusikizwa kwa kesi inayopendekeza aondolewe afisini kuhusiana na hatua ya serikali yake kutwaa Hospitali ya Nakuru War Memorial, zimefeli.

Hii ni baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali ombi lake la kutaka kesi hiyo iliyowasilishwa na Chama cha Mawakili Nchini (LSK), na inayopendekeza iamuliwe kuwa hafai kushikilia afisi ya ugavana.

Jaji Patricia Gichohi, pia alikataa ombi lingine lililomtaka asitishe kusikizwa kwa kesi hiyo hadi kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi nyingine iliyoko katika Mahakama Kuu ya Nyandarua, inayolenga kubaini umiliki wa ardhi ambako kumejengwa hospitali hiyo.

“Kwa hivyo, pendekezo la gavana kwamba kesi hii isimamishwe hadi ile ya Nyandarua ELC E003 ya 2024 isikizwe na kuamuliwa, haina maana na haijakubalika,” akaamua Jaji Gichohi.

Katika kesi ya sasa iliyowasilishwa mnamo Aprili 15, 2024, LSK inaitaka mahakama kuamua kwamba hatua ya serikali ya kaunti kutumia wahalifu kuvamia na kutwaa usimamizi wa Hospitali ya Nakuru War Memorial ilikiuka katiba na inawaaibisha Wakenya.

Aidha, chama hicho cha wanasheria kiliitaka mahakama kuamua kwamba Bi Kihika hafai kushikilia afisi ya ugavana wa Nakuru “kwa kuvumia hospitali hiyo na kuharibu mali ya thamani kubwa kwa nia ya kuficha ushahidi.”

Walalamishi hayo wanasema kuwa kutwaliwa kwa nguvu kwa hospitali hiyo ya serikali ya kaunti ya Nakuru kulisababisha vifo na machungu kwa wagonjwa waliokuwa wakipokea matibabu humo.

Kulingana na LSK wagonjwa wanne waliokuwa hali mahututi walipoteza maisha yao, wagonjwa watatu waliokuwa wakisubiri kupokewa walikataliwa baada ya faili zao kupotea ilhali wengi walioratibiwa kufanyiwa upasuaji hawakupata huduma hiyo muhimu.

Kwa hivyo, walalamishi hao walidai kuwa Gavana Kihiki alikiuka haki za wagonjwa na wafanyakazi wa hospitali hiyo na umma kwa ujumla.

“Kwa hivyo, gavana huyo amekiuka hitaji la Sura ya Sita ya Katiba kuhusu maadili na uongozi,” LSK ikaeleza.

Akijibu, Gavana Kihika alijitetea akisema kuwa Mahakama Kuu haina mamlaka kuruhusu maombi aliyowasilisha kwa sababu kesi hiyo “kesi hiyo inahusu masuala ya umiliki wa ardhi ambayo yanapasa kushughulikiwa na Mahakama ya Mazingira na Ardhi.”