Siasa

Wabunge wa ODM waonya Gachagua, Wamaua dhidi ya kumshambulia Raila

Na CHARLES WASONGA July 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya wabunge wa ODM wamemtaka aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Mbunge wa Mau Mary Wamaua kukomesha kampeni za kuwaharibia jina na kuwatakia mabaya viongozi kutoka jamii ya Waluo wanaohudumu serikalini.

Wabunge hao, Jared Okello (Nyando), TJ Kajwang’ (Ruaraka) na Joshua Oron wa Kisumu Mashariki pia walikerwa na matamshi ya Bi Wamaua yaliyoonekana kumtakia kifo kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Kwa maneno ya Rigathi Gachagua na Mary Wamaua haifa kwa John Mbadi kusimamia Wizara ya Fedha na Opiyo Wandayi anaongoza Wizara ya Kawi kama Waziri. Kwa mtanzamo wa Gachagua na wenzake ni hatia kwa Dkt Raymond Omollo kuhudumu kama Katibu katika Wizara ya Usalama,” Bw Okello akawaambia wanawahabari Julai 1, 2025 katika majengo ya bunge.

“Mary Wamaua amepiga hatua na kusema kuwa jamii yake huomba kwamba Mheshimiwa Raila Odinga afe. Hawaamini kuwa Raila yungali hai na anafanya kazi na Rais Ruto,” akaongeza akisoma taarifa yao.

Wabunge hao kampeni chafu zinazoendeshwa dhidi ya Odinga na viongozi kutoka jamii ya Waluo na wanablogu waliokodiwa na Gachagua, Wamaua na wabunge wengine kutoka Mlima Kenya, zitaambulia pakavu.

“Sasa imebainika wazi kuwa Gachagua anaishambulia serikali kwa sababu ya utendakazi mbaya, bali ni kwa sababu inashirikisha watu kutoka jamii ya Waluo haswa wandani wa Raila,” akasema Bw Okello.

Mbunge huyo wa Nyando alieleza kuwa ni kinaya kwamba Gachagua anaishambulio serikali hii ilhali inayo mawaziri wanane kutoka eneo la Mlima Kenya eneo la Luo Nyanza linawakilishwa na watu wawili pekee katika baraza la mawaziri.

“Tunataka kumwambia Gachagua, Wamaua na wengine wenye fikra sawa na yao kwamba uchungu wanaouhisi wakati huu kuhusu idadi ndogo ya Waluo wanaohudumu serikalini, jamii ya Waluo imepitia uchungu huo tangu taifa hili ilipopata uhuru,” akasema Bw Kajwang.

Mbunge huyo wa Ruaraka alimwonya Gachagua na wenzake dhidi ya kumshambulia Raila akisema kiongozi huyo wa ODM ni mwanasiasa wa hadhi ya juu zaidi kumzidi.

“Inaonekana kuwa Gachagua angali ana machungu kwamba viongozi wa ODM walifanikisha kutimuliwa kwake afisini kupitia mswada uliopitishwa mwaka jana katika bunge la kitaifa na seneti. Ajue kuwa hawezi kushikilia wadhifa wowote wa umma katika taifa hili,” akaeleza Bw Kajwang’.

Kwa upande wake Bw Oron alimtaja Gachagua kama kiongozi wa kikabila na ambaye hawezi kulinganishwa na Bw Odinga mwenye hadhi na heshima kitaifa.

Kauli za wabunge hawa imejiri siku chache baada ya Bw Odinga kumtaja Bw Gachagua kama kiongozi aliyepoteza mwelekeo na ambaye hawezi kufanya kazi nayo.

“Siwezi kufanya kazi na kiongozi ambaye anafananisha serikali na kampuni ambako watu wanamiliki hisa– ambako kuna watu wenye hisa nyingi na wengine wenye hisa chache,” akasema Ijumaa wiki jana katika hafla ya kuchanga fedha katika eneo bunge la Rarieda, kaunti ya Siaya.