Kitendawili ushahidi wa risasi ukikosa kupatikana kwa waliokufa kwenye maandamano
FAMILIA ya marehemu Ian Opango ilisafiri kutoka Kakamega hadi Nairobi, safari ambayo ilijaa huzuni nzito kuliko mizigo waliyokuwa wamebeba.
Walikuwa wakisafiri si tu kuthibitisha jinsi mvulana wao wa miaka 17 alivyofariki, bali pia kuomboleza kifo cha babu yake, Henry Shikanda, aliyepoteza maisha kwa kushtuka baada ya kusikia kuwa mjukuu wake aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Kwa baba yake Ian, Bw Jackson Juma Opango, maumivu anayapitia ni makubwa mno – kupoteza mwanawe na baba yake kwa wakati mmoja.
“Kifo hiki ni kigumu mno. Baba yangu alikufa kwa mshtuko aliposikia kuwa Ian ameuawa. Mwanangu alipigwa risasi na maafisa wa usalama wa serikali. Ikiwa serikali hii ina utu, basi inisaidie kupeleka miili yao Kakamega kwa mazishi,” Bw Juma alisema nje ya Mochari ya Nairobi huku akijizuia kulia.
Karibu naye alisimama mjomba wa babu ya Ian, Bw Harrison Chitechi Sabatia, ambaye alieleza kwa masikitiko jinsi maisha ya kijana huyo yalivyokatizwa mapema sana.
“Opango alikuwa mchanga mno, na alikuwa tu ameenda kumtembelea shangazi yake Rongai. Hakumaliza hata miezi miwili Nairobi na sasa ametangulia. Mzee alishindwa kustahimili mshtuko kwa sababu tayari alikuwa anaugua kiharusi. Habari za kifo cha Ian zilimvunja moyo kabisa na akafariki siku hiyo hiyo tuliyoondoka Kakamega,” alisema.
Mita chache kutoka hapo alisimama Bi Merceline Otieno Kesa, mjane wa Fred Wanyonyi – mlinzi aliyeuawa kwa kupigwa risasi kazini katika afisi za Kenya Power eneo la Parklands.
Bi Kesa alitazama kwa huzuni ripoti ya upasuaji wa mwili wa marehemu mumewe – kile anachosema ndicho kitu pekee cha “faraja” anachoweza kuwa nacho kwa sasa. Mumewe alifariki baada ya risasi kupita tumboni mwake hadi kwenye uti wa mgongo. Hata hivyo, risasi yenyewe haikupatikana.
“Tutapataje haki ikiwa risasi haipo? Mume wangu alipigwa risasi tumboni. Hakukuwa na tundu la kutokea – basi risasi iko wapi? Tutawezaje kujua nani alifanya haya?” aliuliza kwa uchungu.
Marehemu Wanyonyi alikuwa amepandishwa cheo miezi miwili kabla ya kuuawa, na pamoja na mkewe walikuwa wanapanga kununua kipande cha ardhi mwezi Agosti, hatua yao ya kwanza kuelekea maisha salama ya baadaye.
Sasa mjane huyo amesema ameachwa na maswali mengi yasiyo na majibu na jeraha lisilopona.
Rafiki wa familia hiyo, Bw Oscar Wanjala, alisisitiza mashaka yao.
“Tunahisi kuna hujuma. Inawezekanaje risasi itoweke mwilini mwa mtu? Lazima mtu awajibike kwa hili,” alisema.
Wakati familia hizo zikisubiri majibu, familia ya David Mwangi ilijiandaa kwa usiku mwingine wa huzuni.
Kijana huyo wa miaka 19 alipigwa risasi kichwani katika eneo la Imara Daima Jumatano iliyopita, ikisemekana aliuawa na afisa wa polisi wa ngazi ya juu. Madaktari wa upasuaji walichelewesha upasuaji wa mwili wake hadi leo (Jumatano, Julai 2) kutokana na uchovu.
“Tumepasuka mioyo. Tunataka tu kujua ukweli – nani alimuua David na kwa nini? Alikuwa na miaka 19 tu. Alistahili maisha marefu, si jeneza. Tutarudi hapa kesho kwa upasuaji,” alisema mjomba wake John Mwangi.
Katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, familia tatu zingine ziliendelea kuomboleza huku wapendwa wao wakiwa wamewekwa kwenye meza za upasuaji. Abdul Juma aliyefariki Pipeline na Elijah Muthoka aliyeuawa Githurai, wote walipata majeraha mabaya kichwani kutokana na kupigwa kwa nguvu.
Mwathiriwa mchanga zaidi, ambaye uchunguzi wake bado ulikuwa unaendelea, alikuwa msichana wa miaka 14 kutoka Shauri Moyo. Mwili wake mdogo ulikuwa umelala chini ya mwangaza mkali wa hospitali
Mkurugenzi Mtendaji wa Vocal Africa, Bw Hussein Khalid, akizungumza katika Mochari ya Nairobi, alikemea mtindo wa kutisha unaojitokeza kutokana na upasuaji wa miili hiyo.
“Waathiriwa wawili walipigwa risasi kichwani – lakini risasi iko wapi? Tunawezaje kuamini kuwa tutapata haki ikiwa ushahidi unatoweka mochari?” aliuliza.
Alitoa wito kwa Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) kuacha kuchelewesha uchunguzi na kuwawajibisha wahusika.
“Tumepoteza maisha ya vijana wengi – kati ya miaka 14 hadi 22. Hawa walikuwa vijana waliokuwa na ndoto. Na tunapata mwili baada ya mwili bila majibu. Kama IPOA haitachukua hatua, tuna tumaini gani?” aliuliza kwa uchungu.
Pia alimlaumu Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw Kipchumba Murkomen, kwa agizo lake la hivi karibuni kwa polisi kuua waandamanaji karibu na vituo vya polisi jambo lililozua taharuki kubwa kwa Wakenya.
“Agizo hilo lilikuwa la kiholela. Katika nchi ambayo tayari inalia kwa mauaji ya polisi, kuwaambia maafisa wapige watu risasi ili kuua ni hukumu ya kifo kwa vijana. Tunasema: imetosha!” Bw Khalid alisema.
Jana, viongozi wa upinzani walitoa ahadi ya kusaidia familia za waliouawa au kujeruhiwa na polisi katika maandamano ya kizazi cha Gen Z.
Wakati huo huo, walitumia fursa hiyo kurudia wito wao wa kutaka Waziri Murkomen ajiuzulu.
Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa chama cha Democratic Action Party Eugene Wamalwa walitoa ahadi hiyo walipotembelea familia ya Boniface Kariuki, muuzaji barakoa aliyeuawa kwa risasi Nairobi Juni 17 na kufariki Jumatatu.