Habari za Kitaifa

ODM yajitenga na mswada tata wa Esther Passaris wa kudhibiti maandamano

Na SAMWEL OWINO July 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

UONGOZI wa Walio Wachache Bungeni umejitenga na Mswada unaopiga marufuku maandamano uliowasilishwa na Mwakilishi Mwanamke, Nairobi, Esther Passaris.

Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed alieleza Taifa Leo kwamba ODM haihusiki kwa vyovyote na mswada huo.

Sheria hiyo iliyopendekezwa ambayo sasa inakaguliwa na kamati ya bunge kuhusu usimamizi na usalama wa nchi inalenga kutenga maeneo matatu ambapo waandamanaji hawataruhusiwa kushiriki mikutano ya hadhara wala maandamano.

Kulingana na mswada huo, endapo utaidhinishwa kuwa sheria, waandamanaji hawataruhusiwa kuandamana sehemu zilizo umbali wa mita 100 kutoka majengo ya bunge, maeneo yaliyolindwa kama vile ikulu na majengo ya korti.

“ODM haihusiki kamwe na Mswada huo, ni mswada wa mtu binafsi unaomilikiwa na mbunge binafsi sio sisi,” alisema Bw Mohammed.

Bw Mohammed, hata hivyo, alifafanua pendekezo hilo la sheria bado halijakuwa mswada kwa sababu bado halijapita mchakato wote.

“Pendekezo hilo la kisheria bado linahitajika kwenda kwa kamati ya bajeti kutathmini iwapo lina athari kifedha kisha kwa spika atakayeamua iwapo litachapishwa au la,” alisema.

Alipoulizwa ikiwa mswada huo una uwezekano wa kupitishwa bungeni, kiongozi wa wachache alisema, “uwezekano wake wa kupita ni 50-50 tusubiri tuone jinsi mambo yatakavyosonga.”

“Sikubaliani kuwa kubadilisha Sheria kuhusu Utaratibu wa Umma kutabadilisha hali tuliyomo. Ni sharti tuangazie uhalisia unaoangaziwa na watu,” alisema Mbunge Aduma Owuor (Nyakach).