Mwanamume akatwa sikio baada ya kufumaniwa akiwa na mke wa wenyewe
WANAUME wawili wanauguza majeraha kwenye hospitali ya rufaa ya King Fahd kisiwani Lamu baada ya kuvamiwa na kukatwa katika visa viwili tofauti.
Katika kisa cha kwanza, mwanamume wa miaka 25 kwa jina Furaha Karisa alivamiwa kwa upanga na kukatwa sikio lake la kulia baada ya kufumaniwa na mke wa mwenyewe.
Kisa hicho kilitokea kwenye kijiji cha Makafuni B Jumatano asubuhi.
Chifu wa Lokesheni ya Langoni, Bw Haidar Faki, Jumatano aliambia Taifa Leo kwamba mshukiwa aliyemshambulia Bw Furaha kwa jina Karisa Katana, 30, tayari amekamatwa na polisi huku uchunguzi ukiendelea kuhusiana na tukio hilo.
Bw Faki hata hivyo aliwaonya wananchi dhidi ya kujichukulia sheria mikononi mwao punde wanapotofautiana.
“Wawili hao ni watu wa karibu. Wanafahamiana vyema kwani ni mtu na jirani yake kijijini Makafuni B. Katana anadai kutekeleza uvamizi huo dhidi ya Furaha kwani amechoka kumuona akilala na mkewe. Aliyejerhiwa amekimbizwa hospitalini baada ya kuripoti polisi. Katana tayari amekamatwa na anazuiliwa na polisi kwa uchunguzi,” akasema Bw Faki.
Katika kisa cha pili, mwanamume wa miaka 35, Kenga Hussein, pia anauguza majeraha mabaya ya mikononi baada ya kushambuliwa na kukatwakatwa na rafiki yake.
Kisa hicho kilitokea kwenye kilabu kimoja cha pombe mtaani Wiyoni kisiwani Lamu Jumanne jioni.
Naibu wa Chifu wa Lokesheni ya Mkomani, Bw Abdulhakim Ahmed, aliambia Taifa Leo Jumatano kwamba huenda tukio hilo lilichangiwa na ulevi.

Picha|Kalume Kazungu
Bw Ahmed aidha alieleza masikitiko yake kwamba licha ya visa vingi vya watu kushambuliana, kujeruhiana na hata kuuana kwa mapanga kutekelezwa kisiwani Lamu, idadi kubwa huwa haviripotiwi kwa polisi.
“Tumeweka mabaraza ya mara kwa mara kwamba punde kunapokuwa na uvamizi, kujeruhiana na hata kuuana, kabla ya wahusika kufika hospitalini lazima waripoti kwa polisi. Watu hapa wamekuwa wakikwepa kabisa kufika polisi kupiga ripoti wanaposhambuliwa. Yote yanatokana na baadhi ya watu hapa kujihusisha na ulevi wa pombe ya kienyeji, hasa mnazi na mkoma,” akasema Bw Ahmed.
Visa hivyo viwili vinajiri wakati ambapo idara ya polisi kaunti ya Lamu kila mara imejitokeza kuonya wananchi dhidi ya kuendeleza visasi na kuhasiriana.
Kamanda wa Polisi, Kaunti ya Lamu, Bw Kipsang Changach, alisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayepatikana akijichukulia sheria mikononi mwake.
“Hivi visa vya kukatana kwa mapanga na visu mara nyingi hutokana na watu kuwekeana visasi. Lazima watu watii sheria za nchi. Ni hatia kujichukulia sheria mikononi mwako. Tukikupata tutakukamata na kukushtaki,” akasema Bw Changach.