Hatimaye ‘Zico’ afutwa kazi Gor baada ya msimu mgumu
GOR Mahia Jumatano ilivunja benchi yake ya kiufundi baada ya msimu mgumu.
Klabu hiyo ilikosa kushinda taji lolote, hali inayomaanisha sasa itakosa Mashindano ya Afrika (CAF) kwa mara ya kwanza tangu 2016.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Gor kupigwa mabao 2-1 Jumapili katika fainali ya kipute cha Mozzart Bet kwa dhidi ya limbukeni Nairobi United.
Wataalamu wanaofunga virago ni kocha mkuu Zedekiah ‘Zico’ Otieno, naibu wake Michael Nam, mkufunzi wa makipa Boniface Oluoch na meneja wa timu Victor Nyaoro.
Katika, msimu huu uliokamilika wikendi, K’Ogalo walibadilisha makocha mara tatu lakini matokeo uwanjani hayakupendeza hata kidogo ndiposa mashabiki wakatoa wito pawepo mabadiliko.
Mkufunzi raia wa Brazil Leonardo Neiva aliondoka klabuni humo mnamo Novemba 13 baada ya kulemewa na fujo na hata kwa wakati moja kupigwa na mashabiki.
Alikuwa amehudumu kwa miezi mitatu pekee na kuondoka kwake kulihusishwa na kuchimbiwa na baadhi ya benchi ya kiufundi pamoja na mchezaji mmoja katika kikosi cha kwanza.
Kocha raia wa Croatia Sinisa Mihic aliletwa mnamo Februari 3 lakini akaondoka Mei 19 kutokana na tofauti kati yake na Otieno, Nyaoro na Nam. Kisha Otieno na wenzake walichukua usukani hadi msimu ukatamatika.
Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakuzaa matunda huku Gor ikiishia kupoteza ubingwa ambao ulitwaliwa na Kenya Police mbali na kukosa kuwika dhidi ya timu dhaifu kwenye ligi.
“Klabu imevunja benchi yake ya kiufundi pamoja na wanachama wa kitengo chake cha usalama. Hii ni kati ya mbinu ya klabu kujiimarisha na kuanza kujipanga kwa msimu ujao,” ikasema taarifa iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa klabu Ambrose Rachier (ADOR).
Hata klabu ilipovunja benchi yake ya kiufundi, furaha ilikuwa kuhusu kutimuliwa kwa Otieno, jagina wa klabu ambaye amekuwa akiandamwa na ghadhabu za mashabiki.
“Wanasema mimi ndiyo nasababisha Gor isishinde mechi. Niondoke timu niachie nani?” Otieno alikuwa ameambia Taifa Leo Jumanne kabla ya kufutwa jana.
Ilikuwa dhahiri mashabiki hawakuwa wakimtaka Otieno kwa kuwa walimwaandama wakitaka kumpiga baada ya fainali ya Mozzart Bet.
Mahojiano na wachezaji wa Gor yalionyesha jinsi ambavyo klabu hiyo ilikuwa ikipambana na tofauti kati ya benchi ya kiufundi pamoja na kuzozania jinsi ya kupanga timu.