Makala

Mwanaume ateketezwa kwa kumuua mkewe, kuipika nyama yake na kulisha wanawe

Na WYCLIFFE NYABERI July 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIA wenye hasira Kaunti ya Kisii wamemuua kwa kumteketeza moto mwanamume anayesemekana kumuua mkewe na kisha kuipika nyama yake ili ale pamoja na watoto wake wawili.

Tukio hili la kushangaza ambalo limewaacha wengi na mshtuko mkubwa, lilijiri Jumanne asubuhi kijijini Bosansa, Nyacheki katika eneobunge la Bobasi.

Mwanamume huyo aliyetambuliwa kama Stephen Onserio, 55 anadaiwa kumuua mkewe-Evelyne Nyaboke- siku chache zilizopita kwa sababu zisizojulikana.

Baada ya kutekeleza mauaji hayo, Onserio anasemekana kuanza kuzurura kijijini na mmoja wa watoto wake ambaye ni wa umri wa miaka miwili.

Katika kuzurura huko, jamaa huyo alionekana amechanganyikiwa na hivyo basi ikawabidi wenyeji kutaka kufahamu kilichokuwa kinaendelea.

Wanakijiji waliopigwa na butwaa kufuatia habari za Onserio kuua mkewe. Picha|Wycliffe Nyaberi

Kulingana na Bw Boniface Abel, Onserio alihojiwa na wanakijiji na alipokosa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu ni kwa nini alikuwa akiranda randa na mtoto huyo mdogo, wanakijiji walifululiza hadi nyumbani kwake wakiwa na lengo la kubaini kilichokuwa kikiendelea.

Walimuuliza alikokuwa ameenda mke wake ambaye mara nyingi hushinda na wanawe nyumbani.

Walipofika, wanakijiji hao walikaribishwa na uvundo mkali uliokuwa ukitoka ndani ya nyumba ya Onserio.

Walimlazimisha aifungue na pindi tu walipoingia, walivipata vipande va nyama iliyokuwa imepikwa na nyingine isiyokuwa imepikwa ambayo waliamini ni ya binadamu.

“Nyama nyingine ilikuwa imekatwa katwa vipande na nyingine kupikwa. Mtoto wake mkubwa, ambaye ni binti mwenye umri wa miaka 13 mwenye matatizo ya akili, alipatikana akiwa amefungiwa ndani ya nyumba,” Bw Boniface alisema.

Wanakijiji hao walianza kumpiga Bw Onserio na hapo alikiri kuwa nyama hiyo ilikuwa ya mkewe Nyaboke aliyekuwa amemuua.

“Alikiri na kusema kwamba alikuwa akiwapikia watoto wake nyama ya mama yao. Alisema alikuwa ametekeleza mauaji hayo siku chache zilizopita. Baada ya kukiri kwake, wanakijiji waliokuwa na hasira walimvamia na kumchoma moto mita chache kutoka nyumbani kwake,” Bw Boniface aliongeza.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Nyamache Kipkemoi Kipkulei alisema walikimbia hadi eneo la tukio walipofahamishwa kuhusu kilichojiri.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Nyamache Kipkemoi Kipkulei akizungumzia kisa cha Onserio. Picha|Wycliffe Nyaberi

“Tulipokea taarifa kutoka kwa chifu wa eneo hilo na mara moja tukakimbia huko, askari wetu walipofika tulikuta mtu anayedaiwa kumuua mkewe ameuawa na kundi la watu waliokuwa na hasira, tulichakura nyumba yake na tukashtuka kukuta sehemu nyingine za binadamu zikiwa zimekatwakatwa zimefichwa nje ya nyumba ya mtu huyo. Tulipata kichwa cha binadamu na paja lililokuwa limeanza kuoza. Tulipeleka vipande hivyo katika mochari ya Hospitali ya mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH),” Bw Kipkulei alisema.

Bosi huyo wa polisi alifichua kwamba mwanamume huyo aliyeteketezwa alikuwa mfungwa ambaye alirejea nyumbani miaka miwili iliyopita baada ya kutumikia kifungo kingine gerezani cha mauaji ya mke wake wa kwanza.

Kamanda huyo wa polisi alisema kuwa mwanaume huyo alifungwa mwanzo mwaka 2007.

‘Tulibaini kwamba alikuwa amehukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake wa kwanza mwaka wa 2007. Alirejea nyumbani miaka miwili iliyopita na wanakijiji walipomwona akiwa amechanganyikiwa, walifikiri kwamba huenda alikuwa ametekeleza mauaji mengine,” Bw Kipkulei aliongeza.

Taifa Leo ilipozuru nyumbani kwa marehemu hao Jumatano jioni, hali ya huzuni ilitanda. Wanakijiji walijitahidi kukubaliana na kilichotokea.

Onserio na mkewe walikuwa wakiishi maisha ya kujitenga.

Nyumba iliyo katika hali mbovu ambayo Onserio alikuwa akiishi na mkewe na wanawe wawili. Picha|Wycliffe Nyaberi

Bustani ilimokuwa nyumba yao ilikuwa imemea magugu, nyasi na vichaka vingine virefu ambavyo viliacha watu na maswali jinsi binadamu hao walikuwa wakiishi hapo.

Madirisha ya nyumba hiyo ya mabati na udongo yalikuwa yamekomelewa kutoka nje. Ndani ya nyumba, kulikuwa na mrundikano wa kila aina ya vitu.

Wazazi na ndugu zake Onserio walikuwa wamehamia maeneo mengine alipomuua mke wake wa kwanza. Watoto wa marehemu walikuwa wamehamia kwa msamaria mwema-Everlyn Bosibori.

Bi Bosibori alifichua kwamba binti mkubwa wa marehemu wazazi hao, ambaye ni akili punguani alikuwa amepachikwa mimba na mwanaume huyo.

“Wanakijiji walisema kwamba Onserio ndiye aliyempa ujauzito. Kwa kuwa msichana huyo ni wa mahitaji maalum, anahitaji uangalizi wa kutosha na ninatoa wito kwa mtu yeyote anayemtakia heri ajitokeze na kumsaidia,” Bi Bosibori alisema.