Habari za Kitaifa

Familia ya mchuuzi Kariuki iliitwa hospitalini kumuaga kabla ya kufa, afichua mamake

Na STEVE OTIENO July 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAMA mzazi wa muuzaji wa barakoa aliyeuawa kwa kufyatuliwa risasi na afisa wa polisi, Boniface Kariuki, Bi Susan Njeri, anakumbuka vyema simu aliyopokea Ijumaa iliyopita ambayo madaktari wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) walimwambia alete watoto wake Nairobi kumuaga mwanawe kwa mara ya mwisho.

“Walisema tufike ‘kufunga ukurasa’. Watoto watatu wa Kariuki waliruhusiwa kuingia wodini baada ya ushauri, lakini yule wa mwisho ambaye ana miaka saba na yuko Darasa la Pili hakuruhusiwa. Waliambiwa wazungumze naye, waseme chochote walichotaka. Hapo ndipo nilijua mwanangu anafariki,” Bi Njeri alisema katika mahojiano.

Kariuki, mwenye umri wa miaka 22, alikuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi baada ya kupigwa risasi kwa karibu na afisa wa polisi wakati wa maandamano yaliyofanyika jijini Nairobi mnamo Juni 17. Alitangazwa kuwa amepoteza fahamu za ubongo siku ya Jumapili, na siku moja baadaye alifariki dunia.

“Nilipigiwa simu na mtu asiyejulikana,” anasema kwa sauti ya chini. “Alisema Boni amekufa. Nilizimia.”

Sasa, katika kijiji cha Nduni, Kaunti ya Murang’a, huzuni imeikumba familia ya Kariuki kama ukungu mzito. Hewa ni nzito, na sauti ya panga ikikata vichaka vya nyasi imekuwa ya pekee. Jamaa wachache wanazunguka kimya kimya wakisafisha boma endapo kuna mgeni atafika kuleta rambirambi au msaada.

Bw Kimotho Kamau, aliyeketi kimya kwenye kiti cha plastiki, anasema familia haijaathirika tu na msiba huu bali pia imelemewa.

“Kuna bili ya hospitali ya Sh3 milioni. Jamaa tunaowatarajia hawana uwezo. Hata wakija, wataweza kusaidia kivipi?” anauliza.

Hakuna mialiko rasmi iliyotumwa. “Wale watakaokuja, watakuja kwa nia njema tu,” Kamotho anaongeza.

Tangu Kariuki alipofariki, familia haijapokea taarifa yoyote rasmi kutoka kwa serikali. Wanasema wamesikia tu uvumi kuwa huenda serikali ikafuta bili za hospitali kwa waathiriwa wa maandamano.

Anasema mara ya mwisho baba yake Kariuki, Jonna Kariuki, alipozungumza na afisa yeyote wa serikali, aliambiwa kwa maneno tu aandae mchango akisaidiana na familia. Bw Kariuki alikuwa akikesha KNH tangu mwanawe alipolazwa. Sasa anatafuta njia ya kupeleka mwili wa mwanawe nyumbani.

“Alituambia hospitali imesema ikiwa bili italipwa, wanaweza kuhamisha mwili hadi mji wa Kenol, ambao uko karibu zaidi,” Kamotho anaongeza.

Bi Njeri anasema Kariuki alikuwa na ndoto kubwa.

“Alisema angetujengea nyumba, angetuletea umeme na angewasomesha dada zake,” anasema.

Sauti yake inabadilika kuwa kali wakati mada ya haki inatajwa.

“Afisa aliyempiga risasi mwanangu amefunguliwa mashtaka na anatarajiwa kufika kortini Julai 3. Lakini siamini kama kesi hii itaendelea,” anasema.

“Rais alisema hivi majuzi kuwa hataki maafisa wake wa polisi wasumbuliwe. Hiyo inawapa uhuru wa kufanya watakavyo. Hii si haki.”

Wakati wa kujitetea mahakamani, afisa huyo wa polisi alidai alitumia risasi ya mpira. Lakini, Bi Njeri anasema: “Mashahidi waliona maganda ya risasi. Wanaamini alitumia risasi halisi.”