Jinsi wabunge waliungana wote kuhalalisha hazina tatu watakazosimamia na kufaidi
JUMLA ya wabunge 304 Jumanne waliupigia kura mswada unaolenga kuhalalisha kikatiba hazina tatu watakazosimamia kwa lengo la kujifaidi.
Bunge la Kitaifa ambalo nyakati fulani hukosa idadi tosha ya wabunge linaposhughulikia miswada ya kufaidi wananchi liliandikisha historia kwa kuvutia idadi kubwa zaidi ya wabunge walioungana kupitisha mswada huo wa marekebisho ya Katiba.
Aidha, wabunge wa ODM walijasirika kwenda kinyume na msimamo wa kiongozi wao Raila Odinga na kupiga kura ya kuunga mkono mswada huo.
Mswada huo wa Marekebisho ya Katiba ya 2025, unalenga kuhalalisha kikatiba, Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (NG-CDF), Hazina ya Usawazishaji (NGAAF) na Hazina ya Seneti kuhusu Ufutiliaji wa Utendakazi wa Serikali za Kaunti (SOF).
Ingawa sheria ya NG-CDF haiwaruhusu wabunge kusimamia matumizi ya fedha za hazina hiyo, wana usemi katika utoaji wa zabuni kwa miradi inayofadhiliwa na fedha za hazina hiyo. Shughuli hiyo huzongwa na ufisadi na wizi wa fedha za umma inavyofichuliwa kila mwaka kwenye ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Kuna visa ambapo kampuni zinazomilikiwa na wabunge ndizo hupewa zabuni za kutekeleza miradi inayofadhiliwa kwa pesa za NG-CDF.
Ripoti za mkaguzi wa hesabu hufichua visa kadhaa ambapo wanakandarasi hufanya kazi mbovu kwa kuitishwa hongo.
Tayari wabunge kadhaa wanakabiliwa na kesi za ufisadi zinazohusiana na fedha za hazina.
Hazina hiyo ya ustawi wa maeneo bunge ilianzishwa kupitia Sheria ya Ustawi wa Maeneo Bunge ya 2003 iliyoanza kutumika Aprili 2004. Sheria hiyo sasa imefanyiwa marekebisho.
Lengo la hazina hiyo lilikuwa kuanzisha kwa miradi ya maendeleo katika maeneo ya mashinani kupitia mgao wa asilimia 2.5 ya mapato ya serikali ya kitaifa.
Lakini sasa hazina hiyo imekuwa kivutio kwa wale wanaowania viti vya ubunge.
Ni kwa misingi ya NG-CDF ambapo chaguzi katika maeneo bunge 290 hushuhudia ushindani mkubwa zikilinganishwa na chaguzi za maseneta wanaowakilisha maeneo makubwa.
Bw Odinga amekuwa akiwashutumu wabunge kutokana na uchu wao wa kutaka kusimamia fedha hizo katika ngazi za maeneo akisema hiyo ni wajibu wa serikali za kaunti.
Mnamo Novemba mwaka jana, waziri huyo mkuu wa zamani aliwahi kusema kuwa “ni aibu kwamba baadhi ya wabunge ndio wanakandarasi katika miradi inayofadhiliwa na NG-CDF.”
Juzi, Bw Odinga alionya kwamba mwenendo wa wabunge kuendelea kusimamia fedha za hazina hiyo unaibua hali ya muingiliano wa kimasilahi na kuhujumu uwajibikaji.
Alisema mbunge hawezi kukagua utendakazi wa serikali ya kitaifa huku akitekeleza miradi ambayo anatarajiwa kukagua.
“Hazina ya NG-CDF ni njia mojawapo ambayo wabunge wanatumia kuingilia majukumu ya serikali za kaunti. Wabunge hawana wajibu wowote katika ujenzi wa barabara, hospitali na shule,” Bw Odinga akasema.
“Endesheni shughuli za ushirikishaji wa umma kwa mswada huo, mnavyotaka lakini mwishowe, sharti uwasilishwe katika kura ya maamuzi na mtashindwa. Sio kwamba hatutaki basari, zitakuwepo lakini zikisambazwa na serikali za kaunti,” Bw Odinga akaongeza alipofanya mkutano na maseneta katika ukumbi wa Seneti.
Lakini wakati wa kujadiliwa kwa mswada huo mnamo Juni 26, wabunge walipuuza masuala hayo yaliyoibuliwa na Odinga.
Waliunganana kupitisha mswada huo kwa kauli; hamna hata mmoja aliyepinga.
Kila mmoja alitumia lugha mzuri kuelezea mafanikio yaliyopatikana kupitia hazina ya NG-CDF hukuwa wakiwasuta wapinzani wa wake akiwemo Bw Odinga na Baraza la Magavana nchini (CoG).