Habari

Wito Wakenya wachangamkie nyumba za bei nafuu

Na WINNIE ONYANDO July 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

AFISA Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Nyumba Nafuu Sheila Waweru, ametoa wito kwa Wakenya kuchangamkia mpango mpya utakaowawezesha kumiliki nyumba za bei nafuu kwa urahisi.

Akizungumza Jumatano baada ya kukutana na wakazi wa eneo la South B, Nairobi, Bi Waweru alisema kuwa mpango huo ni sehemu ya juhudi za serikali kuondoa vizingiti vinavyowanyima Wakenya hasa wale wa tabaka la chini nafasi ya kumiliki makazi yao wenyewe.

“Tumezindua mpango huu ili kupunguza gharama ya awali ambayo mara nyingi imekuwa kikwazo kwa watu wengi. Kupitia mpango huu mpya, kiwango cha amana kimepunguzwa kutoka asilimia 10 hadi asilimia 5 pekee,” alisema Bi Waweru.

Diwani wa Nairobi Kusini Waithera Chege aliwahimiza wakazi wa eneo lake kukumbatia mpango huo kwani utawasaidia kumiliki nyumba kwa urahisi.

Hapo awali, Bi Waweru alisema kuwa nyumba zote zipo wazi kuchukuliwa kupitia kwa mpango wa ulipaji wa muda mrefu ambao unaruhusu wanunuzi kulipia kwa viwango vidogo kwa muda wa miaka 30.

Haya yanajiri wiki chache baada ya Rais William Ruto kupeana funguo za kwanza chini ya mradi wake wa Nyumba Nafuu katika mtaa wa mabanda jijini Nairobi.

Nyumba hizo 1,080 katika mtaa wa Mukuru zilipewa wamiliki katika hafla ya kufana ambayo Rais alipeana funguo na kuwatakia maisha mema wanapoanza safari ya kumiliki rasilmali jijini Nairobi.

Serikali ilikuwa imesema kwamba wakazi wa Mukuru na Mariguini watapewa kipau mbele katika kugawanya nyumba hizo pindi zitakapokamilika.