Matiang’i ajitenga na uozo wa serikali iliyopita huku akisema yeye si mradi wa Uhuru
ALIYEKUWA Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i, ameanzisha harakati za kujitenga na madai kwamba, alihusika na visa vya ukiukaji wa haki za binadamu alipokuwa akisimamia wizara hiyo yenye nguvu chini ya utawala wa serikali ya Jubilee.
Hasa, Dkt Matiang’i amejitenga na madai kwamba, alihusika na vifo vya kutatanisha vilivyotokea akiwa waziri wa usalama wa ndani, ikiwemo kifo cha aliyekuwa meneja wa ICT katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Chris Msando.
Akizungumza Jumanne jioni katika mahojiano na Citizen TV, Matiang’i alisema alipoondoka serikalini, mauaji ya Msando yalikuwa bado yanachunguzwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).
Kulingana na Waziri huyo wa zamani, licha ya jitihada kadhaa za kufuatilia hali ya uchunguzi huo, DCI iliendelea kumwambia kuwa faili ya uchunguzi wa kifo cha Msando bado ilikuwa wazi kumaanisha haukuwa umekamilika.
Kulingana na Dkt Matiang’i ambaye ametangaza azma ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2027, alipoondoka ofisini, maafisa wa upelelezi pia walikuwa wakifuatilia kesi zingine zikiwemo mauaji ya mfanyabiashara Jacob Juma, ambayo alisema hadi sasa bado yanachunguzwa.
“Kisa kiliripotiwa, nami najua kama vile ninyi mnavyojua – kwamba afisa wa IEBC aliuawa. Uchunguzi ulikuwa unaendelea. Kila mara suala hili linapojitokeza, huwa nasema, ‘Mbona tusifanye uchunguzi wa umma kuhusu jambo hili?’’ Matiang’i alihoji.
“Palikuwa na kesi kadhaa, kama ya Jacob Juma, ambazo pia zilikuwa chini ya uchunguzi. DCI iliendelea kusema kuwa faili bado iko wazi; hata kama wewe ni Rais, hauwezi kuwa na cha kufanya,” aliongeza.
Kuhusu mauaji ambayo miili ilipatikana imetupwa Mto Yala, ambapo miili zaidi ya 30 ilipatikana, Matiang’i alisema kuwa suala hilo lilifikishwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi wakati huo, Hillary Mutyambai, ambaye alimweleza kuwa walihitaji jamaa wa waathiriwa kusaidia katika uchunguzi.
Matiang’i alieleza kuwa, Mutyambai alimwambia kuwa walihitaji familia za waathiriwa kutambua wapendwa wao ili kurahisisha uchunguzi.
Alisisitiza kuwa kufikia wakati alipoondoka ofisini, faili za kesi hizo zilikuwa bado wazi, na jukumu la kufuatilia lilikuwa la serikali ya sasa.
“Tulimuuliza IG Mutyambai kuhusu kilichokuwa kinaendelea wakati huo. Tulikubaliana kuwa suala hilo lilikuwa nzito kiasi kwamba, DCI alipaswa kwenda huko kuona kilichokuwa kikiendelea,” alisema.
“Waliporudi, waliombwa kuanzisha uchunguzi na kufika wakati wetu kuondoka serikalini, faili ilikuwa imefunguliwa. Sikuondoka nayo.”
Kulingana na waziri huyo wa zamani, njia bora ya kushughulikia vifo vya kutatanisha vya zamani ni kufanya uchunguzi wa wazi wa umma ili watu waliokuwa kwenye sekta ya usalama wakati huo waweze kutoa taarifa muhimu kuhusu masuala hayo.
Alipoulizwa kuhusu utajiri wake na iwapo yuko tayari kuutangaza hadharani, Matiang’i alipuuza swali hilo akisema halina umuhimu wowote.
“La, sijui thamani ya mali yangu ni gani, na hata kama ningejua, si suala la kujadiliwa na umma kwa sababu mimi si afisa wa umma na ninyi si tume ambayo natakiwa kutangazia mali zangu,” alisema.
Aliongeza, “Tangu nizaliwe, sijawahi kuwa juu ya sheria, hata nilipokuwa waziri, sikuwa juu ya sheria.”
Matiang’i alisisitiza kuwa, analenga kuunda muungano na vyama kadhaa vya kisiasa ili kuongeza nafasi yake kupata ushindi kuongoza nchi baada ya uchaguzi wa mwaka 2027.
“Bila shaka, tunapoendelea mbele, haitakuwa chama kimoja pekee kitakachounda serikali. Ningependelea kuwa na mashauriano ya kina na Wakenya kutoka nyanja mbalimbali kabla sijasema rasmi huu ndio mtindo nitakaotumia kuwasilisha azma yangu kwa IEBC,” alisema Matiang’i.
Waziri huyo wa zamani pia alisema anafurahi kumezewa mate na vyama mbalimbali vya kisiasa vinavyotaka kumpa tiketi ya kugombea urais.
“Nimealikwa na vyama vya kisiasa saba au nane vikiniuliza iwapo tunaweza kushirikiana. Inafurahisha kuona kuwa, tuna viongozi wengi wa kisiasa wanaoketi kwenye kamati zao kuu na kusema vinataka Fred Matiang’i awe mgombea wao, hata kabla sijawaomba,” Matiang’i alisema.
Matiang’i amekuwa akionekana katika mrengo wa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa chama cha Peoples Liberation Party Martha Karua, Kiongozi wa Chama cha Democratic Party Justin Muturi, Kiongozi wa Chama cha DAP-Kenya Eugene Wamalwa, na Chama cha Jubilee miongoni mwa wengine.
Ingawa chama cha Jubilee, kinachoongozwa na Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta, kimetangaza kitamuunga mkono waziri huyo wa zamani katika kinyang’anyiro hicho, Dkt Matiang’i anashikilia kuwa “ni mapema kwangu kuteua chama nitakachokitumia.”
“Nafanya mashauriano na vyama kadhaa vya kisiasa na viongozi kadhaa wa kisiasa. Naamini kwamba nikifanya chaguo sasa na kuegemea chama kimoja cha kisiasa, sitakuwa nikitenda haki kwa wengine ambao tunajadiliana nao,” akasema Dkt Matiang’i kwenye mahojiano na runinga ya Citizen Jumanne usiku.
Hata hivyo, Dkt Matiang’i, ambaye pia aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Elimu, Kaimu Waziri wa Ardhi na Waziri wa ICT wakati wa utawala wa Bw Kenyatta, alikariri kuwa angali mwandani wa karibu wa rais huyo mstaafu.
“Hata hivyo, hiyo hainifanyi kuwa mradi wa Uhuru kwani rais huyo hushirikiana na viongozi wengine wengi wakiwemo wale wanaohudumu katika serikali ya sasa,” akaeleza.