Habari

Visa vya ulawiti na ubakaji vyaongezeka South B wakazi wakitakiwa kupiga ripoti

Na WINNIE ONYANDO July 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAKAZI wa eneo la South B Nairobi wanaishi kwa hofu huku visa vya ulawiti, ubakaji na dhuluma zingine za kimapenzi vikiongezeka.

Katika juhudi za kukabiliana na visa hivyo, diwani wa Wadi ya South B, Bi Waithera Chege akishirikiana na viongozi wengine wa kijamii wamezindua kampeni ya pamoja ya kukabiliana na visa hivyo vya unyama.

Akizungumza wakati wa kikao na wakazi wa eneo hilo kilichohudhuriwa pia na maafisa wa usalama na wawakilishi kutoka Muungano wa mawakili wanawake FIDA-Kenya, Bi Waithera alisisitiza kuwa ni lazima haki itendeke kwa waathiriwa.

“Hatutakubali watoto wetu kuendelea kunyanyaswa kimapenzi. Tunahitaji ushirikiano ili kuhakikisha kuwa wahalifu wanatambuliwa na kufikishwa mahakamani,” alisema Bi Waithera.

Naye Mkuu wa Kituo cha Polisi cha South B, Mohamed Nuur, aliwahimiza wakazi kushirikiana nao kikamilifu ili kutoa ripoti kwa wakati kuhusu matukio yoyote ya kutiliwa shaka.

“Tunaomba msiogope. Ripoti kila kisa kwa haraka. Kwa pamoja tunaweza kuzuia haya matukio kabla hayajazidi,” alisema Nuur.

Kwa upande wao, maafisa wa FIDA walitoa elimu kuhusu masuala ya ubakaji na ulawiti, wakifafanua hatua ambazo waathiriwa wanaweza kuchukua ili kupata haki.

Walieleza pia kuhusu mchakato wa kisheria na umuhimu wa kujitokeza kupiga ripoti.

Wakazi waliohudhuria kikao hicho walikaribisha juhudi hizo wakitaka mikakati thabiti kuwekwa ili kuwalinda watoto na vijana dhidi ya visa kama hivyo.

“Ni jambo la kusikitisha sana kuona watoto wakidhulumiwa. Tunahitaji viongozi wetu na maafisa wa usalama kuwa macho na kuchukua hatua za haraka dhidi ya wahusika,” alisema mama mmoja mkazi wa South B.

Wito umetolewa kwa wazazi, walimu na viongozi wa kidini kushirikiana kwa karibu katika kulea watoto kwa maadili na kuwaelimisha kuhusu hatari ya unyanyasaji wa kingono.