Mtasubiri sana tutengane lakini hatuachani, upinzani wasema wakiwa Magharibi
VIONGOZI wa upinzani jana walishikilia kuwa hawapo chini ya shinikizo zozote za kutaja mwaniaji wao wa urais, huku wakiahidi kuwa muungano wao mpya hautapasuka kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Wakiongea maeneo mbalimbali Magharibi mwa Nchi, viongozi hao walisema suala la nani atapeperusha bendera yao si hoja ila wanamakinikia kumfanya Rais William Ruto ahudumu kwa muhula moja pekee.
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya jana walikita kambi Magharibi mwa Nchi ambako ambako walieleza imani ya kushinda kura ya 2027.
“Hiki ni kikosi cha kuhakikisha kuwa Rais Ruto anahudumu muhula mmoja pekee wala hatuna shinikizo zozote za kumtaja mgombeaji wetu wa urais mapema. Tunataka kuhakikisha kuwa tuna kikosi imara na atakayepeperusha bendera yetu atakuwa tu sawa na vinara wengine kwenye muungano huu,” akasema Bw Musyoka.
Makamu huyo wa rais wa zamani alikanusha vikali madai kuwa kuna mgawanyiko kati yao akisema hiyo ni ishara kuwa wapinzani wao wameingiwa uoga.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunawaokoa Wakenya kutoka utawala huu na hatuwezi kuwasaliti raia ambao wengi wao wameweka imani kwetu. Sote tuko kwenye msafara huu na hiyo ni ishara kuwa tuko pamoja,” akasema Bw Musyoka.
Kauli ya Bw Musyoka inakuja baada ya Gavana wa Kisii Simba Arati kudai kuwa kuna baadhi ya viongozi katika kambi ya upinzani ambao walikuwa wanakosea wenzao heshima.
Wito huo huo wa umoja ulikaririwa na Dkt Matiangí pamoja na Bw Wamalwa huku pia wakidai serikali ndiyo imekuwa ikifadhili uharibifu unaofanyika wakati wa maandamano.
Baada ya kuhutubia kikao cha wanahabari uwanja wa ndege wa Kisumu, walifululiza hadi Luanda na Kakamega ambako walihutubia wafuasi wao kisha wakamalizia mikutano yao Kisumu Mashariki.
Mjini Kakamega, Dkt Matiangí alimshutumu Gavana Ferndandes Baraza kwa kujaribu kutumia wahuni kuwazuia kuhutubia wafuasi wao.
Hii ni baada ya baadhi ya vijana kuwasha moto barabarani na kuwakabili viongozi hao wa upinzani kisa ambacho karibu kiishie kwa fujo.
“Barasa kama Mkenya yeyote ana haki ya kusaka kura eneo lolote na atakaribishwa. Anastahili kujua Wakenya wengine pia wana haki ya kufika Kakamega bila kuzuia. Ni aibu kwa mtu kufikiria kuwa baada ya miaka 60 ya uhuru bado mji wa Kakamega ni mali yake kibinafsi,” akasema Dkt Matiangí.
Kuhusu siasa za Magharibi, Bw Wamalwa alisema jamii ya Mulembe haitawaachwa nyuma kwenye jitihada za kumwondoa Rais Ruto madarakani.
“Mnamo 2002 Waluhya walijiunga na jamii nyingine na tukaondoa serikali ya Moi. Mnamo 2027, historia itajirudia na Rais Ruto ataenda nyumbani,” akasema Bw Wamalwa.